KUNA mambo matatu yatatazamwa katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa leo Alhamisi kati ya Simba na Fountain Gate kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kwanza, Fountain Gate inaingia katika mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 tu, kati ya hao makipa ni wawili, hivyo inaweza kutokea yaliyotokea misimu miwili iliyopita wakati Azam ikiikabili Kitayosce iliyokuja kufahakika kama Tabora United na sasa ikibadili tena jina na kuwa TRA United.
Katika mchezo huo wa kwanza msimu uliopita ambao Azam ilishinda mabao 4-0, Kitayosce iliingia na wachezaji wanane kufuatia changamoto ya usajili. Hata hivyo, mechi hiyo ilimalizika kikanuni katika dakika ya 15 baada ya wachezaji wawili wa Kitayosce kuumia na kushindwa kuendelea hivyo kufanya kubaki sita.

Jambo la pili katika mechi hiyo ni kuhusu kocha Seleman Matola anayeiongoza tena Simba kucheza mechi ya ligi baada ya kufanya hivyo Septemba 7, 2022 katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa alipokabidhiwa mikoba kufuatia kuondoka ghafla kwa Zoran Maki.
Jambo la tatu ni kwamba Fountain haijawahi kuifunga Simba katika mechi sita walizokutana katika Ligi Kuu tangu timu hiyo ilipokuwa ikiitwa Singida Big Stars kisha kuwa Singida Fountain Gate baada ya kununuliwa.
Kitendo cha kutopoteza mechi yoyoye dhidi ya Fountain Gate tangu kukutana kwao, kinaipa jeuri Simba kwa pambano la leo linaloanza saa 1:00 usiku, huku Matola akisisitiza jambo.
Fountain inaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka kupoteza nyumbani kwa bao 1-0 mbele ya Mbeya City ikiwa ni mechi ya kwanza ya ligi msimu huu.
Mara ya mwisho Simba na Fountain Gate kukutana ilikuwa Juni 2, 2025 katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati Manyara ambako matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1, lakini katika mechi ya kwanza iliyokuwa na mazingira kama ya msimu huu ya kutokamilisha usajili wa wachezaji, jamaa walichezea kichapo cha mabao 4-0.

Hata hivyo, wakati mara ya mwisho timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 pia zinakutana leo zikifahamu kwamba kila moja mechi ya mwisho katika ligi imepoteza.
Ipo hivi. Fountain Gate inakwenda kucheza mechi ya pili ya ligi msimu huu baada ya ile wa kwanza kufungwa 1-0 dhidi ya Mbeya City, lakini Simba ni mchezo wa kwanza huku ikiwa imemaliza msimu uliopita kwa kichapo cha mabao 2-0 mbele ya Yanga.
Rekodi zinaonyesha, Fountain Gate tangu ilipokuwa ikifahamika kwa jina la Singida Big Stars, kisha Singida Fountain, timu hiyo imeambulia sare mbili pekee dhidi ya Simba ambazo zimepatikana katika mchezo wa kwanza na ule wa mwisho matokeo yakiwa 1-1, huku ikipokea vichapo vinne katika Ligi Kuu Bara tangu msimu wa 2022-2023. Haijawahi kupata ushindi.
Matokeo ya mechi sita za ligi walizokutana yapo hivi; Fountain Gate 1-1 Simba (Juni 02, 2025), Simba 4-0 Fountain Gate (Agosti 25, 2024), Simba 3-1 Fountain Gate (Machi 12, 2024), Fountain Gate 1-2 Simba (Oktoba 08, 2023), Simba 3-1 Fountain Gate (Februari 03, 2023), Fountain Gate 1-1 Simba (Novemba 09, 2022).

Benchi la ufundi la Simba litaongozwa na kocha Seleman Matola, ambaye amechukua majukumu hayo baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids.
Akizungumzia utayari wa kikosi cha Simba kwa mechi hiyo, Matola alisema: “Tupo tayari na tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu katika mchezo wetu wa kwanza wa ligi.”
Matola amezungumzia kuondoka kwa Fadlu akisema: “Si mara ya kwanza kitu kama hiki kutokea, sisi ni profeshno sambamba na wachezaji wote wa Simba, hii imeshatokea na imeshapita, kikubwa tunaangalia mchezo wetu wa kesho (leo) kupata matokeo mazuri.
“Tanzania tumekuwa na ligi ngumu na bora kabisa, kwa hiyo naweza kusema haitakuwa mechi rahisi, ukiangalia Fountain Gate walipoteza mchezo uliopita, hivyo hawatataka kupoteza kwa mara ya pili, ukiangalia unaona kabisa mchezo utakuwa mgumu na umuhimu kwa kiasi gani, lakini tunataka tuanze vizuri ligi.
“Malengo yetu ni kupata kikombe hiki kwa hiyo lazima tuanze vizuri kesho (leo). Pamoja na ugumu wa Fountain Gate na kupoteza kwao mechi ya kwanza, tumejipanga kuhakikisha tunachukua alama zote tatu katika mchezo huu.”
Kwa upande wa Fountain Gate, kocha mkuu wa kikosi hicho, Denis Kitambi, ametaja ugumu anaokutana nao katika maandalizi kufuatia changamoto inayoikabili timu hiyo ya kuwa na wachezaji wachache baada ya kukwama katika mfumo wa usajili.
“Maandalizi ya mechi dhidi ya Simba kwa kweli ni magumu kutokana na changamoto tunayopitia kuhusiana na idadi ya wachezaji ambao wapo tayari kutumika kwa mchezo wa kesho (leo).”
Hata hivyo, Kitambi amebainisha hawataingia kinyonge, kwani wana malengo ya kufanya vizuri baada ya kuyafanyia kazi matatizo yaliyojitokeza mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City.
“Malengo yetu makubwa kama benchi la ufundi tumeelekeza katika kutatua changamoto zilizojitokeza katika mechi dhidi ya Mbeya City na pia namna gani tunaweza kuwatumia wachezaji waliopo dhidi ya mpinzani wetu wa kesho (leo).
“Dhidi ya Mbeya City tuliona kuna mabadiliko ya kiuchezaji, timu imekuwa ikienda mbele vizuri kushambulia jambo ambalo mwanzo lilikuwa changamoto, kilichobaki sasa zile nafasi ambazo tunazitengeneza tuzitumie ukizingatia mpinzani tunayekwenda kukutana naye Simba sidhani kama tutatengeneza nafasi nyingi kama ilivyokuwa dhidi ya Mbeya City.”

Licha ya Fountain kuwa ugenini na idadi ndogo ya wachezaji, bado Kitambi alisema hawana presha kubwa, huku akieleza wapinzani wao ndiyo watakuwa kwenye presha ya kupata ushindi.
“Kila mechi ina presha, lakini mchezo wa kesho (leo) sidhani presha kama ipo kwetu bali ipo kwa Simba kwani ndiyo wengi wanaipa nafasi kubwa ya kushinda mchezo. Sisi tunachotaka ni kuonyesha kiwango kikubwa pamoja na changamoto tunazopitia. Imani yangu ni kwamba kwa siku tulizojiandaa basi tutajitahidi,” alisema Kitambi.
Changamoto inayokumbana nayo Fountain Gate ni kuwa na wachezaji 14 pekee kutokana na kukutana na tatizo la kiufundi katika mfumo wa usajili wa kimataifa (TMS) ilipokuwa ikiingiza majina kabla ya usajili kufungwa Septemba 7 mwaka huu. Pia wachezaji wanne waliumia katika mechi iliyopita.