Mambo yamnyookea Simbu jeshini, sasa ni Sajinitaji

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda amempandisha cheo, Sajini Alphonse Simbu kuwa Sajinitaji (Staff Sergeant) baada ya kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya mbio za marathon ya kilomita 42 yaliyofanyika Tokyo, Japan.

Simbu amepandishwa cheo leo, Alhamisi Septemba 25, 2025 katika Makao Makuu ya Jeshi Upanga, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika tukio hilo, Jenerali Jacob Mkunda amesema ushindi wa Simbu ni fahari kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla na kwamba michezo ni sehemu ya kazi za kijeshi, hivyo ni mfano wa kuigwa na askari wote.

“Ushindi huu si wa Simbu pekee, bali ni wa Jeshi na Taifa lote. Ameonyesha nidhamu, bidii na uzalendo, mambo ambayo kila askari anapaswa kuyaiga,” amesema Jenerali Mkunda.


Aidha, amewataka maofisa na askari wote kujifunza kutoka kwa Simbu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kila idara jeshini inaleta matokeo chanya.