Mbeya. Mgombea urais wa chama cha Demokrasia Makini (Makini), Coaster Kibonde amesema akipata nafasi ya kuongoza nchi, serikali yake itatoa chakula bure kwa wanafunzi wote nchini na kuifuta Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Amesema anahitaji kuona mabadiliko katika sekta ya elimu kwa kujenga nchi iliyo na wasomi na wajuzi wenye kujiajiri, kuajiri na kuajiriwa ndani na nje ya nchi na kujenga viwanda vitakavyozalisha ajira za kutosha.
Akizungumza leo Septemba 25, 2025 katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, amesema serikali yake itakuwa ya mabadiliko katika maeneo ya elimu, kilimo na afya.
Amesema kwa namna mwitikio ulivyo katika mkutano wake kwa wananchi wa Ubaruku, inampa ishara kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itaenda kumtangaza Oktoba 29, 2025 akiahidi kuwa ahadi yake ni kulipa maendeleo.
“Novemba 5 ndio nitaenda kula kiapo cha urais, ahadi yangu kwenu vijana kuanzia miaka 21-35, tutatoa ekari tano na hati miliki, hii itasaidia kuondokana na umasikini, tumegundua wakulima ni wengi hapa Mbarali lakini wanazalisha kidogo.
“Tutaleta mbegu kutoka nje ya nchi ambazo kwa ekali moja mkulima atavuna gunia 240, tutaleta kilimo cha umwagiliaji, visima vya maji ili kuondokana na kutegemea kilimo cha mvua, nawaomba mnipe kura ili nitimize ahadi hizi na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja,” amesema.
Ameeleza kuwa akipata kura za ushindi atapambana na migogoro ya ardhi kwa wakulima wilayani humo na kutafuta soko la uhakika nje ya nchi kwa bei ya juu na kutakuwa na uhuru wa mkulima kuuza bidhaa hiyo nchini Canada.
Amesema suala la amani na utulivu kwa Tanzania itakuwa sehemu ya utekelezaji wake katika uongozi wake akieleza kuwa mgawanyo na migogoro yoyote inapotokea waathirika zaidi ni wanawake na watoto, akiwaomba wananchi kuwapinga wanaohatarisha amani na utulivu nchini.
“Nimeonana na bodaboda na mamalishe walionipa kero zao, kwamba wapo askari wa barabarani wasio waaminifu kuwanyanyasa, hivyo nipeni ridhaa ili niwe Amiri Jeshi Mkuu, nitoe amri moja kwa askari hawa wasiwanyanyase vijana.
“Tutatoa bodaboda milioni moja kwa kuanzia, anzeni mafunzo mafupi ya udereva ili tufanye mazungumzo na Jeshi la Polisi muweze kupata leseni na pikipiki hizo bure, tutajenga kiwanda kikubwa cha pembejeo na tutatoa bure kwa wakulima,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza, Azza Haji Suleiman amesema bado uzalishaji bidhaa ni mdogo na ndio maana bei ya vitu inakuwa ghali, akihoji wakulima kutopata tija katika kilimo.
Amesema mazao yanayozalishwa hayajawa bora katika kukidhi viwango, akieleza kuwa suluhisho ni kukipa chama cha Makini ridhaa kuongoza nchi ili kuleta mabadiliko.
“Tumefanya tafiti lazima tuwe na nyenzo bora tutaanza na zao la mchele kuuzwa kwa Sh 800 kwa kilo, lakini ikiwa ni kwa uzalishaji bora ili bidhaa hii iuzwe hata nje ya nchi kwa kuingia kwenye masoko.
“Tupeni nafasi tuibadili sekta ya Kilimo, tunahitaji pia amani kwa ajili ya maendeleo yetu, tusiichezee amani ambayo ndio itatufanya kuyafikia malengo,” amesema Azza.
Awali, naibu katibu mwenezi wa chama hicho Taifa, Ramadhan Bambo amewashukuru wananchi kwa muitikio wao wa kuhudhuria mkutano huo kwa ridhaa yao bila ushawishi wowote akieleza kuwa hiyo ni ishara tosha Oktoba 29, wagombea wao kushinda.
“Sisi hatujaja na wasanii kama walivyo wengine na kutoa kofia kwa wananchi, ujio wenu huu kwa mwitikio mkubwa unamaanisha namna mnakubali chama chetu na Oktoba 29, mnaenda kutupa ushindi,” amesema.
Mgombea ubunge wa Ubungo, Grace Nyonyani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Makini Bara, amesema mabadiliko ni sasa, hivyo ili kufikia malengo ni kuchukua hatua.
“Baadhi ya nchi za jirani wameshajua ahadi za vyama tawala, sasa basi hatma yetu Watanzania ni Oktoba 29 kuondokana na ahadi hewa zisizotekelezeka, wamepita wengi pimeni sera mkafanye uamuzi,” amesema Grace.