Mwalimu abisha hodi Tunduma na ahadi ya ujenzi wa barabara ya juu

Tunduma. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ametoa ahadi mbili kwa wakazi wa Mkoa wa Songwe ikiwemo ya kujenga barabara ya juu (flyover) kuanzia eneo la Mpemba hadi mpaka wa Zambia endapo atapatiwa ridhaa na wananchi ya kuwa rais katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano,  Oktoba 29 mwaka huu.

Mbali na hilo, Mwalimu ambaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho, ameahidi kuanzisha Jiji la Tunduma kama hatua ya kimkakati ya kuimarisha biashara ya mipakani, utalii na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.

Akizungumza leo Alhamisi Septemba 25, 2025 na wakazi wa Kata ya Songea Tunduma katika mkutano wa kampeni, Mwalimu amesema lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano mkubwa wa malori yanayoingia na kutoka nje ya nchi.

Amesema msongamano huo unaathiri biashara, usalama na maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

 “Tutajenga barabara ya juu kuanzia Mpemba hadi mpakani na Zambia. Nataka magari yakiingia yapite moja kwa moja.”

Haya mambo yanawezekana. Nendeni Kenya mkaone wenzetu wamejenga kilomita kwa kilomita, sisi tunashindwaje? Haiwezekani lori likiharibika kidogo tu, foleni tayari,” amesema Mwalimu.


Ameongeza kuwa foleni ya malori inayoanzia Mpemba hadi Laela si tu changamoto ya usafirishaji, bali ni kikwazo kikubwa kwa uchumi wa Taifa kwa kuwa ucheleweshaji wa mizigo unamaanisha ucheleweshaji wa mapato kwa nchi.

Katika kulinganisha vipaumbele vya maendeleo, Mwalimu ameeleza kuwa serikali zilizopo zimekuwa zikiwekeza kwenye miradi ya anasa kwa wachache badala ya maeneo yenye tija ya kiuchumi kwa wananchi wengi.

“Leo kuna daraja Dar es Salaam kutoka Posta hadi Masaki walifanya hivyo ili mawaziri wasikae kwenye foleni. Badala yake, wangetazama barabara ya Tunduma inayoingiza mamilioni ya fedha,” amesema.

Kuhusu kuanzia Jiji la Tunduma

Mwalimu amesema eneo hilo lina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha kibiashara katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kutokana na ukaribu wake na mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na nchi nyingine jirani.


“Ili tuweze kubadilisha mazingira hapa, lazima tuanzishe kitu kinachoitwa Jiji la Tunduma ili liweze kusaidia watu wanaotoka DRC, Zambia na nchi nyingine jirani,” amesema Mwalimu.

Amebainisha kuwa kupitia kuanzishwa kwa jiji hilo, huduma muhimu zitapatikana moja kwa moja Tunduma, na wageni kutoka mataifa mbalimbali watahudumiwa hapo bila kuhangaika kusafiri kwenda maeneo mengine.

Katika kuonyesha tofauti ya kimtazamo kati ya chama chake na serikali ya sasa, amesema:

“Tuna hewa nzuri ya kiuchumi tofauti na CCM ambao akili zao bado za kizamani. Nchi nyingine sehemu kama Tunduma ni ya utalii, burudani, kula starehe. Watu wanaweza kutoka maeneo ya mbali kuja kula raha.”

Mgombea udiwani wa Kata ya Uwanjani, Tunduma kupitia chama cha Chaumma, Michael Kibona amesema dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo ni kuhakikisha anapata nafasi ya kuingia kwenye Baraza la Halmashauri ili kuziba mianya yote inayokwamisha maendeleo, na kuhakikisha mji wa Tunduma unainuka kiuchumi.

“Nataka kuingia kwenye Baraza la Halmashauri kwenda kuwawakilisha wananchi wa Kata yangu ya Uwanjani, kuwasemea na kubwa zaidi kupigania maendeleo kwa kuziba mianya inayofaidisha wachache,” amesema Kibona.

Rebeka Kasanga, mgombea mwingine wa udiwani kupitia Chaumma, amesema chama hicho kinapeleka watu wenye weledi na dhamira ya kweli katika vyombo vya maamuzi, akisisitiza kuwa yuko tayari kutetea masilahi ya wananchi wa mji wa Tunduma.


Kwa upande wake John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa umma wa Chaumma na kiongozi wa msafara wa mgombea urais wa chama hicho, amewataka wananchi wa Tunduma kufanya maamuzi ya mabadiliko kwa kutokiruhusu chama tawala kuendelea kuiongoza Halmashauri ya Tunduma kama kweli wanataka maendeleo.

“Ukiona mji unasuasua kiuchumi, tatizo si wananchi bali ni uongozi. Tunduma inahitaji uongozi mpya wa Chaumma, unaosikiliza na kutatua kero za watu,” amesema Mrema.