Dar es Salaam. Mwili wa Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, aliyekuwa Balozi wa Papa nchini New Zealand unaagwa leo Septemba 25, 2025 mjini Vatican.
Askofu Mkuu Rugambwa alifariki dunia Septemba 16, 2025 akiwa Roma, nchini Italia.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Vatican, misa kwa ajili ya kumwombea na kuaga mwili wake inafanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na Watanzania wengi waishio Italia, kabla ya kusafirishwa kuleta nchini Tanzania kwa maziko.
Akizungumza na Mwananchi Septemba 21, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Jovitus Mwijage alisema wanatarajia mwili huo utasafirishwa kesho Ijumaa, Septemba 26 kuletwa nchini Tanzania.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), katika taarifa ya mazishi ya Askofu Mkuu Rugambwa Septemba 19, lilisema misa ya kumuaga itafanyika Septemba 27, Dar es Salaam.
“Sekretarieti ya TEC inawafahamisha makardinali, maaskofu wakuu, maaskofu, mapadri, watawa na waamini wote kuwa misa ya kumuaga Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, itafanyika katika Kanisa Kuu Ia Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam, Jumamosi Septemba 27, saa 3:00 asubuhi,” ilisema taarifa hiyo.

TEC katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Padri Clement Kihiyo kwa niaba ya katibu mkuu wa baraza hilo, ilimesema misa ya mazishi ifanyanyika kwenye Kanisa Kuu la Jimbo la Bukoba, Jumatatu Septemba 29, saa 3:30 asubuhi.
Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, 1957, katika Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania. Baada ya masomo na majiundo ya kikasisi, alipewa daraja takatifu ya upadri mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.
Alijiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican Julai mosi, 1991.

Baada ya kufanya kazi mbalimbali katika balozi za Vatican, Juni 28, 2007 Papa Benedikto wa XVI alimteua kuwa katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalumu.
Februari 6, 2010, Papa Benedikto XVI, alimteua kuwa Askofu Mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe, akiwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican kwa wakati huo, Machi 18, 2010.
Machi 5, 2015 aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras. Machi 29, 2019, Papa Francisko alimteua kuwa Balozi wa Vatican nchini New Zealand na mwakilishi wa kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific.
Machi 30, 2021, Papa Francisko alimwongezea majukumu kwa kumteua kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific.

Wakati huohuo aliendelea kuwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga. Pia Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, Palau na Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific.
Juni 10, 2025, akiwa mgonjwa Askofu Mkuu Rugambwa alishiriki mkutano wakati Papa Leo XIV, alipokutana na mabalozi wote wa Vatican wanaomwakilisha maeneo yote duniani. Alikuwa akitumia kitimwendo.