Lindi. Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan amehitimisha kampeni zake za siku mbili mkoani Lindi, akiwaahidi wakazi wa mkoa huo kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa gesi asilia.
Mkoa huo unakuwa wa 15 kwa mgombea huyo kupitia akinadi ilani ya CCM na kuomba ridhaa ya urais kwa miaka mitano ijayo, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akihutubia maelfu wa wakazi wa mkoa wa Lindi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Ilulu, Samia amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za makubaliano kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ambao uwekezaji wake unagharimu dola za Marekani bilioni 40.
“Natambua kiu ya Watanzania wengi kuona mradi wa gesi asilia unaanza kutekelezwa. Mradi huu ni mkubwa sana utakaogharimu dola bilioni 40, hivyo anayewekeza lazima awe na uhakika pesa yake anayokuja kuwekeza itamzalishia kitu gani.
“Sisi pia tunaoletewa mradi ni lazima tuwe na uhakika utatuletea nini na maliasili yetu inayokwenda kutumika. Kwa maana hiyo tumekuwa na mizunguko ya mazungumzo, tumezungumza sana kwa miaka miwili sasa tunakaribia kukubaliana,”amesema na kuongeza:
“Tukishakubaliana tutasaini mkataba na wataanza pilika za mradi, ninachotaka kuwaambia wana Lindi mradi upo lakini tusingeweza kupokea mradi bila kuwa na uhakika wa manufaa kwa nchi yetu lazima tuzungumze tujue tunaendaje.”
Katika mkutano huo, CCM kimepokea wanachama wanne kutoka vyama vya upinzani akiwemo aliyekuwa mgombea ubunge wa Mchinga kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Yusuph Tamba na aliyewahi kuwa mbunge wa Lindi Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), na sasa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Lindi mjini, Salum Baruani.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Tamba amesema, “Nilikuwa mgombea pekee mwenye nguvu wa upinzani nikijitutumua, lakini leo yamenishinda baada ya kuiona Ilani ya CCM na kuhisi najidanganya na kuwadanganya wananchi wa jimbo la Mchinga.
“Mimi kama mwanao, kwa heshima na taadhima na kwa ridhaa yangu mwenyewe siku ya leo, ninaunga mkono jitihada za CCM na ninawaomba wananchi wote wa Mchinga tumuunge mkono Samia.
“Natuma salamu kwa chama changu, meseji zimeingia za vitisho nawaambia mimi sitishiki, nimeamua kurudi nyumbani naomba CCM mnipokee,” amesema Tamba akiwa amepiga magoti.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Baruani amesema baada ya kupitia ilani za vyama vyote vya siasa, amebaini ilani ya CCM ndiyo itakayoufungua Mkoa wa Lindi.
“Hakuna chama kilichokuja na ilani ya kuifungua Lindi, ndani ya ilani hii umezungumziwa mradi wa gesi. Mradi huu una miaka 12 tangu nikiwa mbunge lakini hadi leo haujawa tayari.
“Kwa mujibu wa ilani hii, naamini Lindi inaenda kufunguka, tutakuwa wezi wa fadhila kama watu wa Lindi hatutakuunga mkono. Umekuja na hoja ya katiba mpya hiki ndio kilio cha Watanzania wengi, tukupe nini zaidi ya kura zetu,” amesema Baruani.
Akizungumzia ugeni huo Samia amesema, “Niwashukuru wenzetu walioungana nasi leo, kuungana nasi ni jambo moja, lakini waliyoyaeleza ni mazito sana, nawashukuru kwa maoni yao wameona hivyo na wameona waungane nasi.
“Ni imani yangu wenzao ambao bado wana roho za kukereketwa wakiwasikia hawa, basi na wao roho zao zinakuwa zinapoa na Mungu anawapa utulivu wa nyoyo ila wote tuungane na Tanzania yetu twende nayo kwa salama, amani na utulivu.”
Akinadi sera zake kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuomba ridhaa ya miaka mitano ya urais, Samia amesema mkoa huo unaenda kupata vyuo vitatu ambavyo ni ndaki ya kilimo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo inajengwa ndani ya Manispaa ya Lindi na kampasi ndogo ya chuo hicho inayojengwa Ruangwa na chuo cha ufundi.
Katika sekta ya umeme amesema kazi kubwa imeshafanyika ya kuunganisha vijiji vyote na nusu ya vitongoji hivyo akipata ridhaa ya miaka mitano mingine atakwenda kumalizia nusu ya vitongoji vilivyosalia ikiwemo vya mkoa wa Lindi.
Kwenye sekta ya madini amesema mpango uliopo ni kupima nchi nzima ili kubaini maeneo yenye madini kuwawezesha vijana wengi wakiwemo wa mkoa wa Lindi kuingia kwenye sekta hiyo kipaumbele kikiwa wachimbaji wadogo.
Kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama amesema tayari wamefikia lengo la asilimia 87 kwa nchi nzima, akieleza mpango ulipo ni kumaliza kabisa tatizo la maji na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za majisafi na salama.
“Nipongeze kazi iliyofanyika hapa Lindi, ni sahihi kabisa kusema tunakwenda kuufungua mkoa huu na ukanda wote wa kusini. Tunakuja kujenga kiwanja cha ndege hapa Lindi,”amesema Samia.
Kwenye eneo la barabara amesema katika ilani ya CCM 2025,2030 Lindi itaenda kupata barabara zinaounganisha mkoa na wilaya.
Kuhusu wanyama waharibifu amesema Serikali imeanza kulifanyia kazi kwa kuongeza idadi ya askari wa wanyapori ili kuwazuia wanyama wasitoke maeneo ya hifadhi, na mpango ulipo ni kununua ndege nyuki kwa ajili ya kuwafukuza wanyama hao.
Wabunge waomba kura za CCM
Mgombea ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Lindi, Kijakazi Yunus katika kipindi cha miaka minne kiasi cha Sh82 bilioni zimepelekwa katika mkoa huo kuboresha huduma za afya.
“Tumepata zahanati, vituo vya afya na huduma zimeboreshwa katika hospitali zetu za wilaya na mkoa, kwa sababu hii wanawake wa mkoa wa Lindi tutakulipa kwa kura nyingi zitakazokuwezesha kupata ushindi wa kishindo,” amesema Kijakazi.
Mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Mshamu Munde amesema wilaya hiyo imepata zaidi ya Sh140 bilioni zilizotumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo maji, elimu, afya na umeme.
Mgombea ubunge wa jimbo la Kilwa Kusini, Hasnain Dewji ameshukuru kwa Kilwa kupata bandari ambayo ujenzi wake utakamilika miezi sita ijayo huku akiwataka wakazi wa mkoa wa Lindi kutumia fursa ya uwepo wa bandari hiyo kujikwamua kiuchumi.
“Hii ni fursa kubwa kwetu wana Lindi kupitia bandari hii meli kubwa zitakuja, Msumbiji, Kenya, Somalia wataleta samaki wao hivyo kutakuwa na soko kubwa Kilwa,” amesema Dewji.
Mgombea ubunge wa jimbo la Lindi Mjini, Mohamed Utaly amesema tangu Tanzania ipate uhuru Lindi ilikuwa na hospitali moja ya Sokoine lakini katika kipindi cha uongozi wa Samia mkoa huo sasa una hospitali tatu.
Katika sekta ya elimu amesema mkoa huo umepata shule mpya tano, ukamilishaji wa madarasa sita katika shule za sekondari, ikiwa pamoja na bweni la wanafunzi katika shule ya watoto wenye mahitaji maalumu.