Serikali kujadili utitiri wa tozo kwenye zao la parachichi Njombe

Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema atakutana na halmashauri zote za mkoa huo kujadili na kuondoa tozo na ushuru ambao umekuwa kero kwa wakulima.

Hatua hiyo inatokana na malalamiko ya wakulima kwamba halmashauri zimekuwa zikitoza ushuru wa mazao licha ya kushindwa kuboresha miundombinu muhimu ya kuinua kilimo, ikiwemo maji, umeme, barabara na mawasiliano.

Akizungumza leo Septemba 25, 2025, wakati wa kufungua mkutano wa wadau wa parachichi ulioashiria kuanza kwa msimu wa ununuzi, Mtaka amesema haoni sababu ya kutoza ushuru kwa mazao ambayo gharama zote za uzalishaji hubebwa na mkulima.

“Sijaona mantiki ya kutoza ushuru wa parachichi. Kila kitu kuandaa shamba, kukopa, kununua miche na kuwalipa vibarua ni gharama za mkulima. Akipata hasara ni yake, lakini ninyi mnakuja mwaka huu kusema ushuru ni kiasi hiki bila kuchangia chochote,” amesema Mtaka.

Amesema baada ya uchaguzi atakutana na mabaraza ya madiwani kujadili suala hilo na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato, akisisitiza kuwa mkoa huo una rasilimali nyingi zinazoweza kutumika badala ya kuminya wakulima.

Aidha, amewataka watendaji wa Serikali mkoani humo kupunguza urasimu na vikwazo vinavyokwamisha kilimo na kuwaumiza wakulima.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dk Stephen Nindi amesema wizara inaendelea kufanya maboresho makubwa ya sheria, kanuni na taratibu ili kuondoa vikwazo katika biashara ya parachichi.

“Wakulima na wadau wa parachichi mna nafasi kubwa ya kuishauri Serikali ili kuboresha mifumo ya kisera na kisheria, kwa kuwa biashara hii ni fursa kubwa kimataifa. Tumefanya vizuri Afrika Kusini, lakini tunapaswa kupanua nafasi yetu duniani,” amesema Dk Nindi.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Horticulture for Health and Wealth (TAHA), Dk Jacqueline Mkindi amesema sekta ya parachichi imekua kwa asilimia 101 tangu mwaka 2021/2022, kutoka tani 17,700 hadi tani 35,600 zinazouzwa nje ya nchi.

“Ni dhahiri tumepiga hatua kubwa, lakini kazi bado ipo mbele yetu ili kulinda sekta hii na kuhakikisha Tanzania inatawala masoko makubwa ya kimataifa,” amesema Dk Mkindi.

Baadhi ya wakulima walioshiriki mkutano huo, akiwemo Frank Msuya, wameitaka Serikali kuboresha zaidi miundombinu ya maji, umeme na barabara ili kurahisisha maendeleo ya kilimo cha parachichi.

“Tunaomba Serikali izingatie suala la maji ya uhakika na kupunguza vikwazo vinavyotuzuia kusonga mbele,” amesema Msuya.