Stand United yaja na tamasha kusaka mdhamini

Tamasha la Siku ya Wana linatarajiwa kufanyika 0ktoba 04, 2025 likiambatana na michezo mbalimbali, ikiwemo mechi nne za mwanzo huku Stand United ikikabiliana na timu ya Ligi Kuu Bara itakayotajwa hapo baadaye.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 25, 2025, mwenyekiti wa tamasha hilo, Chrispin Kakwaya, amesema: “Timu ya Stand United inaadhimisha Tamasha la Siku ya Wana litakalofanyika Oktoba 04, 2025 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni ambapo tutaanza na mazoezi ya mwili (Jogging), siku hiyo pia wadau wengine wajitokeze kwa wingi ili kusaidia kuidhamini timu yetu ya Stand, milango ya wadhamini iko wazi.

“Siku hiyo kutakuwa na mechi nne za mwanzo ambazo ni timu ya Madereva Bajaji dhidi ya Madereva Bodaboda, Soko Kuu vs Soko la Kambarage, Upongoji FC vs Ibinzamata FC na Stand United dhidi ya timu ya ligi kuu itakayofamika hivi karibuni.”

STAN 01


STAN 01

Naye Ofisa Habari wa Stand United, Ramadhan Zoro, ameeleza kuwa kwa sasa timu yao imejipanga vya kutosha.

“Kwa usajili tulioufanya, kipigo tutakachoruhusu ni kimoja tu, kupigwa picha tu, timu yoyote itakayocheza na sisi ijipange, pia tunaomba mashabiki na watu wote wajitokeze kwa wingi kushuhudia usajili tulioufanya,” amesema Zoro.

Tamasha hilo limedhaminiwa na wadau wanne wa michezo ikiwemo serikali ya wilaya na mkoa, huku kiingilio kikiwa ni Sh5,000 kwa mzunguko, Sh10,000  VIP, pia kutakuwa na tiketi maalumu kwa ajili ya VVIP.