Geita. Uwepo wa tafiti za kijiolojia zinazowawezesha wachimbaji kuchimba maeneo yenye uhakika, pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini yanayohifadhi kumbukumbu za mauzo, umetajwa kuwa kichocheo cha taasisi za fedha kuanza kuwakopesha wachimbaji wadogo.
Akizungumza leo Alhamisi, Septemba 25, 2025, kwenye Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema hatua hizo zimewajengea wachimbaji uaminifu wa kifedha.
“Zamani mchimbaji akienda benki akiwa na leseni pekee hakuwa anakopesheka. Sasa hivi akienda na taarifa za tafiti au rekodi kutoka soko la madini, benki inamwamini. Masoko hayo yana kumbukumbu za kiasi cha dhahabu alichouza kwa mwezi au mwaka, hivyo benki ikihitaji kujiridhisha hupata takwimu rasmi,” amesema Shigella.
Ameongeza kuwa ongezeko la mitambo ya utafiti na uwepo wa maabara za kisasa za kupima sampuli za udongo kumeondoa ubahatishaji na kuongeza ufanisi katika uchimbaji.
“Kwa sasa wachimbaji hawachimbi kwa mazoea, bali kwa kufuata taarifa sahihi. Hii imejenga uaminifu mkubwa kwa taasisi za fedha,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya Stanbic Tawi la Geita, Hilda Gwimba amesema benki hiyo imekwishatoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 100 kwa sekta ya madini ili kuwaunga mkono wachimbaji wadogo na wakubwa.
“Tunaangalia mnyororo mzima wa thamani, kuanzia wachimbaji, watoa huduma migodini hadi wafanyabiashara wa vito vya thamani. Tunakopesha vifaa vya uchimbaji, mitambo mikubwa na hata watoa huduma kwa kutumia mikataba yao na migodi bila dhamana,” amesema Gwimba.
Hata hivyo, Katibu wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Geita (Gerema), Misana Jeremia, amesema bado wachimbaji wengi wanakosa mikopo kutokana na kutokuwa na rekodi za kibenki.
“Wengi wetu bado tunatunza fedha mikononi au kupitia simu. Hali hii ikifanya benki zikihitaji taarifa za kifedha, zinashindwa kuziona. Tukipewa elimu juu ya umuhimu wa kutumia benki, changamoto hii itaondoka na tutakopesheka zaidi,” amesema Jeremia.
Kwa mujibu wa wadau, kuimarika kwa mifumo ya taarifa kupitia tafiti na masoko ya madini kunatarajiwa kuongeza ushirikiano kati ya wachimbaji na taasisi za fedha, na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya madini pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Takwimu zinaonyesha sekta ya madini imekua kwa asilimia 10.6 na kuchangia asilimia 10.1 ya pato la taifa, huku Mkoa wa Geita ukiendelea kuongoza kwa uzalishaji wa dhahabu nchini.
Kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, sekta ya madini mkoani humo imezalisha ajira zaidi ya 35,000 kwa vijana na wanawake.
Wachimbaji wadogo wamezalisha kilo 22,000 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Sh3.4 trilioni na serikali ikipata mapato ya Sh235.5 bilioni kupitia mrabaha na kodi mbalimbali.
Aidha, migodi mikubwa ilizalisha kilo 76,500 za dhahabu zenye thamani ya Sh11.8 trilioni na kuiingizia serikali mapato ya takribani Sh793 bilioni.
Kwa miaka minne iliyopita, wachimbaji wadogo pekee mkoani Geita wamezalisha tani 22.5 za dhahabu, huku migodi mikubwa ikizalisha tani 74.