Dar es Salaam. Kanisa Katoliki nchibni Tanzania limewapiga marufuku watawa, mapadri na waseminari kujihusisha na kampeni za uchaguzi za chama chochote cha siasa, wala kuvaa sare zao ili kulinda heshima na usafi wa kanisa hilo.
Wito huo umetolewa leo Septemba 25, 2025 na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, wakati wa maadhimisho ya jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Seminari ya Kipalapala iliyoko mkoani Tabora.
Akihubiri wakati wa misa ya maadhimisho hayo, Askofu Pisa amezungumzia somo la Biblia katika kitabu cha Wamakabayo kuhusu mama na wanawe walivyoifia imani yao, amewataka watawa, mapadri na waseminari kufanya vivyo hivyo kulinda heshima ya kanisa.
Amewataka kutokubali kanisa lidhoofishwe, walinde usafi wake na kulinda yale yote wanayopaswa kuyalinda.
Amesisitiza kwamba, mwaka huu ni wa uchaguzi, hivyo bila kuamsha hisia za watu, wao wanaelewa nafasi ya kanisa, mapadri wafanye nini, watawa na kiongozi yeyote wa kanisa afanye nini.
Kwa hiyo, amesema sheria za kanisa ziko wazi kila kiongozi afanye nini.
“Sista, mtawa au padri, au kiongozi yeyote wa kanisa, hapaswi kushiriki katika kampeni zozote za siasa, wala hapaswi kutambulishwa na chama chochote kwa kuvalishwa gwanda lolote la chama fulani cha siasa au kiashiria chochote,” amesema na kuongeza:
“Kwa hiyo, ni marufuku mapadri, marufuku kwa watawa, marufuku kwenu nyinyi waseminari, kuonekana kwenye kampeni za siasa. Marufuku kubwa, hatutakiwi kuonekana huko na ni vibaya watu kurubuni na kuhadaa watu wakipita kwenye nyumba za kanisa.”
Akitoa ujumbe rasmi kwa waseminari wa Kipalapala, amewaambia ni marufuku kwao kuvaa fulana au kofia ya chama chochote hata wakati wa michezo au wakati wa kulala usiku, hata kama mgombea ni kaka yake.
Amesema kama mtu anampenda mgombea au chama fulani, basi siku ya kupiga kura wakawapigie wagombea hao baada ya kutafakari dhamiri zao kwanza.
“Kama wagombea wanafikiri wana wafuasi huku (kanisani), haina shida, siku ya kupiga kura inaeleweka. Kama wewe ni mfuasi, basi kapige kura siku hiyo, isipokuwa tunakumbusha kabla ya kwenda huko tathmini kidogo dhamiri yako,” amesema akisisitiza ni kinyume na sheria za kanisa.
Kwa mujibu wa Sheria ya kanisa,
Canon 285 (3), wahudumu wa dini (clerics) wamekatazwa kuchukua nyadhifa za umma zinazohusisha ushiriki katika utekelezaji wa mamlaka ya kiraia.
Canon 287 (2), hawapaswi kushiriki moja kwa moja katika vyama vya siasa au katika kuongoza vyama vya wafanyakazi isipokuwa pale ambapo, kwa uamuzi wa mamlaka ya kikanisa yenye uwezo, inalazimu kwa ajili ya kulinda haki za Kanisa au kuendeleza manufaa ya wote.
Askofu Pisa amesema: “Dhamiri inaweza kuwa potofu kama hakuna uelewa wa kutosha… tuachane na dhamiri potofu. Uwe na uelewa wa kutosha wa hicho unachokwenda kufanya, usikilize dhamiri yako kuhusu ukweli na lililo la haki.”
Kauli hiyo ya Askofu Pisa imetolewa siku moja baada ya picha kusambaa zikiwaonyesha watawa wa kanisa hilo kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika jana Septemba 24, Ndanda, wilayani Masasi mkoani Mtwara, wakiwa wameshika bendera na baadhi wakiwa wamevaa skafu za chama hicho.
Kuhusu uchaguzi, Askofu Pisa amewataka wahudumu wa kanisa hilo kusali na kujihoji dhamiri zao kabla ya kufanya uamuzi wa kwenda kuchagua viongozi wakiwa wanajua lililo la kweli na haki, huku akisisitiza haja ya kumshirikisha Mungu katika uchaguzi wa viongozi.
Amesema watu wakitaka kuliangamiza kanisa, huanza na viongozi wa juu kabla ya kushuka chini, hivyo amewataka wasikubali kanisa kudhoofishwa, bali walinde usafi wake.
Misa hiyo ya jubilee imehudhuriwa na maaskofu, mapadri, masista, watawa na waseminari.