Uhamiaji yafungua Ligi Kuu Zanzibar kwa rekodi mbili

LIGI Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026 imeanza leo kwa kufanyika mchezo mmoja huku ikishuhudiwa Uhamiaji ikiweka rekodi mbili.

Mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, Uhamiaji imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi.

Rekodi ya kwanza Uhamiaji imeiweka kupitia mchezaji wake, Mohamed Mussa kufunga bao la kwanza la msimu akifanya hivyo dakika ya 32. Pia Uhamiaji imekuwa timu ya kwanza mchezaji wake kuonyeshwa kadi nyekundu, adhabu ambayo amekumbana nayo Ali Issa.

Uhamiaji ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0, lakini kipindi cha pili kilianza kwa mabadiliko ya kiufundi kwa Polisi kumuingiza kiungo Rashid Mohammed ambaye alileta uhai wa timu eneo la kati lililoonekana kuzidiwa kipindi cha kwanza. 

Hata hivyo, juhudi za mabadiliko hayo hazikuzaa matunda upande wao ambapo dakika 90 zilimalizika kwa Uhamiaji kumaliza wababe kwa bao 1-0.

Ligi hiyo itaendelea kesho Ijumaa ambapo Junguni United itaikaribisha Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, saa 10:15 jioni.