Dar/Pemba. Wakati mwili wa mgombea ubunge wa Fuoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abbas Mwinyi, ukitarajiwa kuzikwa kesho Septemba 26, 2025, vyama vya siasa vimetuma salamu za rambirambi kwa familia ya hayati Ali Hassan Mwinyi kufuatia msiba huo.
Abbas ambaye ni kaka mkubwa wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amefariki dunia leo Septemba 25, 2025, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu utaratibu wa mazishi ya Abbas, mdogo wa marehemu, Abdullah Mwinyi, amesema ndugu yao atazikwa Mangapwani katika makaburi ya familia, alikozikwa baba yao, Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
“Maziko yatakuwa Mangapwani, Kaskazini Unguja, mwili utasaliwa Masjid Qaboos, baada ya sala ya Ijumaa, na baada ya hapo tutaelekea Mangapwani kuzika. Kule makaburini alikozikwa mzee wetu, mzee Mwinyi,” amesema Abdullah.
Kutoka na msiba huo, chama cha ACT-Wazalendo kimesitisha mkutano wa hadhara na ratiba nyingine za kampeni zilizopangwa kufanyika leo Alhamisi Septemba 25, 2025, ili kuomboleza msiba wa Abbas.
Ratiba ya kampeni ya ACT-Wazalendo ilionesha kuwa mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alitakiwa kufanya mkutano wa hadhara wa kunadi sera zake katika Jimbo la Bumbwini.
Katika taarifa yake kwa umma, Katibu wa Idara ya Habari, Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Salim Biman, amesema kutokana na msiba wa Abbas ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Fuoni, wameamua kusitisha ratiba hiyo.
“Kwa kuzingatia utu, mshikamano na heshima ya kibinadamu, chama cha ACT-Wazalendo kimeamua kusitisha shughuli za kisiasa katika eneo hilo ili kutoa nafasi kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi wote kushiriki katika mazishi na kumzika kwa heshima stahiki mpendwa wao.
“ACT-Wazalendo inaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Bumbwini katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” ameeleza Biman.
Biman amesema ACT-Wazalendo kitatoa tarehe mpya ya mkutano baada ya mashauriano na viongozi wa ngazi ya Taifa ya chama hicho.
Kwa upande wake, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha Kapteni Abbas.
Mwalimu ametoa salamu hizo leo Septemba 25, 2025, akiwa Tunduma mkoani Songwe, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kuomba ridhaa ya kuongoza Serikali.
“Nimepokea taarifa za kuondokewa na kiongozi na mbunge mstaafu wa Fuoni, Kapteni Abbas Ali Mwinyi, ambaye pia alikuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia CCM. Hili ni pigo si kwa familia ya Mzee Mwinyi pekee, bali kwa familia nzima za Zanzibar na taifa kwa ujumla,” amesema.
Mwalimu ameeleza kuwa Kapteni Abbas alikuwa mtaalamu mahiri aliyebobea katika masuala ya fani ya usafiri wa anga na baharini.
“Abbas alikuwa ni mmoja wa watu wachache waliobobea kwenye masuala ya ndege na meli. Hakuwa na makelele, alikuwa mpole, msikivu na mwenye weledi mkubwa. Mungu alimjalia vipaji viwili—urubani na nahodha wa meli,” amesema.
Akiendelea kueleza masikitiko yake, Mwalimu ameongeza kuwa amekuwa akijaribu kupanga ratiba yake ili kama itawezekana, ahudhurie mazishi hayo.
“Nimejulishwa kuwa mazishi yanafanyika kesho. Nitaangalia kama ratiba yangu itaniruhusu kufika, lakini kama itashindikana, familia ijue kwamba tuko nao pamoja katika kipindi hiki kigumu,” amesema.
Katika salamu zake za pole, Mwalimu amewafariji wanafamilia wote wa marehemu, akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, pamoja na uongozi mzima wa CCM kwa kuondokewa na kada na kiongozi wao muhimu.
“Zaidi ya familia, nawapa pole wananchi wa Fuoni kwa kumpoteza aliyekuwa mwakilishi wao. Pamoja na tofauti zetu za kisiasa, Kapteni Abbas alikuwa kiongozi aliyeheshimika,” amesisitiza Mwalimu.
Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ameahirisha shughuli zake za kiserikali huko Pemba kutokana na taarifa za kifo cha kaka yake, Abbas, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Lumumba, Unguja.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwasili Unguja akitokea Pemba kufuatia kifo cha kaka yake, Kapteni Abbas Ali Mwinyi, kilichotokea leo Septemba 25, 2025.
Baada ya kutokea taarifa za msiba huo, Dk Mwinyi aliyekuwa Pemba kwa shughuli za kampeni na kiserikali, amelazimika kuondoka kisiwani humo na kurejea Unguja mapema asubuhi.
Katika ratiba yake ya leo, Dk Mwinyi alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kumkabidhi mkandarasi ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba na barabara ya Chake – Mkoani yenye urefu wa kilometa 43.5.
Baada ya Rais Mwinyi kuondoka, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amemwakilisha katika hafla hiyo.
Imeandikwa na Peter Elias, Jesse Mikofu, Tuzo Mapunda na Bakari Kiango.