Wasira ataja ishara ya ushindi kwa CCM uchaguzi mkuu

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema kuwa Watanzania wako tayari kwa uchaguzi na kwamba, idadi wanaoshiriki kwenye mikutano ya hadhara kusikiliza sera za wagombea ni ishara tosha.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 25, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni kunadi sera za chama hicho, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Amesema mikutano ya kampeni hususan ya chama na ya mgombea urais wao, Samia Suluhu Hassan inaidhihirishia dunia kwamba, Watanzania wako kwenye uchaguzi na wanashiriki kikamilifu.

“Dunia inaona namna watu wanavyokwenda kusikiliza hoja na sera za maendeleo kwenye mikutano ya wagombea wetu. Tuko tayari kwa uchaguzi na hapa tumekuja kutafuta kura za wagombea wetu wa urais, ubunge na udiwani,” amesema Wasira.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah amesema kazi iliyofanywa na Serikali ya chama hicho inatosha kukiwezesha siyo kuibuka na ushindi tu, bali utakuwa wa kishindo.


Rajabu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amesema ujenzi na utekelezaji wa miradi mikubwa na ya mkakati kwa Mkoa wa Tanga, umeufanya mkoa huo kupiga hatua huku uboreshaji wa bandari ukichochea ukuaji wa uchumi wake.

 “Hapa kwetu Tanga hatuna shaka na ushindi wetu kabisa, Kazi kubwa imefanyika hapa na wananchi wanaiona na wanaikubali. Tunachotarajia ni ushindi wa kishindo,” amesema Rajab.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 huku vyama vya siasa takribani 19 vinashiriki vikiwa na uwakilishi kwenye nafasi za urais, ubunge na madiwani.