Ahadi tata za wagombea zawaibua wasomi

Dar es Salaam. Wakati kampeni za vyama vya siasa zikizidi kupamba moto nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, wasomi wamebaini pengo kati ya ahadi zinazotolewa na baadhi ya wagombea na uwezekano wa kutekelezeka.

Pengo hilo limewafanya wanataaluma hao kuona haja ya kufanya mdahalo  Septemba 28, 2025 jijini Dar es Salaam utakaovikutanisha vyama vya siasa, wasomi pamoja na wananchi kujadili ilani za vyama hivyo.

Mdahalo huo ambao utafanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umelenga kuwapa fursa wanataaluma na wananchi kwa ujumla kukutana na viongozi wa vyama husika, ili kuwasikiliza wakichambua ilani za vyama vyao, kisha washiriki kuuliza maswali na kuomba ufafanuzi juu ya mipango iliyobainishwa katika ilani hizo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Septemba 26, 2025, Katibu wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (Udasa), Dk Dominikus Makukula amesema kwa muda wa takribani mwezi mmoja tangu kampeni zilipoanza (Agosti 28) wamebaini mambo kadhaa katika ahadi zinazotolewa na wagombea wa ngazi zinazowaniwa.

Dk Makukula amesema wamebaini baadhi ya ahadi zinazotolewa na wagombea ni ngumu kutekelezeka, huku nyingine zikiwa haziendani na mahitaji halisi ya sasa ya wananchi na zipo ambazo utekelezaji wake unawezekana.

Amesema wameona kuna haja ya kuwakutanisha wananchi, wanataaluma na wanasiasa kupitia makatibu wa vyama hivyo ili kuhoji na kupata ufafanuzi wa mipango iliyopo katika ilani za vyama vyao.

Ameeleza ilani ni orodha ya mambo yote ya ukweli na yanayotekelezeka, ambayo mgombea huyaeleza mbele ya watu pale anapowaomba ridhaa ya kuwaongoza.

“Ilani zinapoelezwa mbele ya umma zinalenga kuwasilisha sera za vyama husika, kushawishi na ni mkataba kati yake na wananchi na wana wajibu wa kutekeleza kile walichokiahidi kwa wananchi,” amesema.

Amesema si kila mwananchi ana uwezo wa kuchambua ilani za vyama vya siasa kitaalamu, hivyo katika mchakato wa uchaguzi wao kama wanataaluma jukumu lao ni kuhakikisha wanatoa elimu na kufanya tafiti ili kuwasaidia wananchi kuelewa.

“Tunatakiwa kumsaidia mwananchi wa kawaida pale chama cha siasa kitakapokuja na ushawishi wenye maneno na ahadi ambazo hazitekelezeki aweze kubaini ili wanaposhawishiwa basi iwe kwa yale ambayo ni ya hakika, kweli na yanatekelezeka,” amesema.

Vilevile, amewahimiza wananchi kuwa na tabia ya kusoma maandiko na uchambuzi unaofanywa na wanataaluma.

“Sisi siyo wanasiasa, tunapoona mambo hayafanyiki au hayaendi sawa, huwa tunaandika katika magazeti na machapisho rasmi kukosoa na kuelimisha umma na wataalamu wengine, wakiwamo watunga sera baada ya kujiridhisha kwa kufanya tafiti,” amesema.

Mwenyekiti wa Udasa, Profesa Elgidius Ichumbaki, amesema lengo la kufanya mdahalo si kuvishambulia vyama vya siasa, bali kuvipa jukwaa la kunadi ilani zao, nini watafanya endapo watapata ridhaa ya kuiongoza Tanzania.

“Sisi Udasa tunatambua kwamba ili chama kiweze kupata ridhaa ya wananchi, lazima kieleze kinaga ubaga ni nini kitafanya ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu na jumuishi,” amesema

Amesema wanalenga kuwasaidia wananchi kuelewa na hatimaye kufanya uamuzi sahihi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Pia, wanawaandaa wanataaluma ambao ni wabobezi katika taaluma ya sayansi ya siasa na tasnia ya habari, ili waweze kuhoji na kutoa maelezo zaidi juu ya kitu gani kilipaswa kufanyika na kutoa ushauri.

Ameeleza pia ni fursa kwa vyama vya siasa kusikia maoni ya wananchi ambao ndio walengwa.

Makamu Mwenyekiti wa Udasa, Profesa Daniel Shilla, amesema wanatamani kuamsha fikra kwa wananchi waweze kuwa na uelewa juu ya umuhimu wa ilani hizo za vyama vya siasa.

Hatua hiyo ya Udasa, imeelezwa na  wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa imekuja wakati muafaka na inaweza kubadilisha namna Watanzania wanavyoshiriki katika siasa.

Mtafiti wa masuala ya utawala, Dk Asha Mwapamba, amelieleza Mwananchi kwamba, mdahalo huo utawasaidia wapigakura kutofautisha kati ya maneno ya kampeni na uhalisia.

“Kampeni mara nyingi hujaa ahadi kubwa, nyingine zikiwa karibu na ndoto. Jukwaa kama hili ambalo vyama vitahojiwa na wanataaluma na wananchi, ni muhimu. Litawezesha wapigakura kufanya uamuzi sahihi kulingana na mambo ambayo ni halisi,” amesema.

Naye Joseph Mtebe, mchambuzi wa kisiasa, amesema hatua ya Udasa ni “Mabadiliko makubwa.”

Amesema: “Watanzania wengi hupiga kura kwa kuongozwa na hisia au ufuasi wa vyama. Mdahalo huu utaonyesha utekelezekaji wa ilani. Iwapo wananchi wataelewa kwamba ilani ni mkataba wa lazima, watapiga kura kwa hekima zaidi.”

Amesema muda wa tukio hilo, ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya uchaguzi, unawapa wapigakura nafasi ya kutafakari vya kutosha.

Katika kampeni zinazoendelea, ukiacha sera zilizoainishwa katika ilani za vyama vya siasa, kumekuwa na ahadi binafsi za wagombea, baadhi zikiibua mijadala ndani ya jamii, ikielezwa hakuna ufafanuzi wa mbinu za utekelezaji wake.

Wengine katika mjadala huo wanasema baadhi ya ahadi utekelezaji wake unahitaji mabadiliko makubwa ya kisheria.

Miongoni mwa ahadi ni kama vile ujenzi wa bwawa la mamba Ikulu, kilimo cha mabungo (matunda) ni zaidi ya karafuu, uhalalishaji wa kilimo cha bangi, ubwabwa kabla ya dripu kwa wagonjwa, posho ya Sh500,000 kila mwezi, mshahara wa Sh700,000 kwa wazee wote, ujio wa Arnold Schwarzenegger Arusha, kuondoa vitanda vya futi sita na ununuzi wa matrekta milioni 400.

Katibu Mkuu wa UPDP, Hamadi Mohamed Ibrahim, akizungumza na Mwananchi amesema amepata taarifa kuhusu mdahalo huo na chama chake kitashiriki na yeye akiwa katibu mkuu atakiwakilisha chama hicho.

“Suala la kutekelezeka kwa ahadi zetu tutalijadili huko, lakini tunaamini hakuna jambo ambalo halitekelezeki. Watu wanatoa ahadi kwa sababu tunatafuta nafasi ya kuongoza nchi, Serikali haijawahi kushindwa kitu,” amesema.

Katibu Mkuu wa Ada-Tadea, Saleh Msumari amesema chama chake kina taarifa za mdahalo huo, lakini changamoto ni kwamba, yeye ni meneja wa kampeni za mgombea wa urais wa chama hicho. Hata hivyo, amesema amethibitisha kushiriki mdahalo huo.

“Wao wanasema ahadi zisizotekelezeka lakini mtu ukipewa nchi ni ahadi zinazotekelezeka. Ada-Tadea tumeandaa ilani moja nzuri na bora kabisa, endapo Mungu akitujalia tukafanikiwa kushinda, ni ilani ambayo inatekelezeka,” amesema na kuongeza:

“Unajua watu wanaona ni vitu visivyotekelezeka kwa sababu nchi imejaa upendeleo, ufisadi na rushwa lakini tuna vitu vingi ambavyo Mungu ametujalia, mfano tuna madini ya Tanzanite, tukisema madini haya kazi yake ni kulipa deni la Taifa tu, inawezekana.”

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Abdalla Mohammed amekiri kuwa na taarifa za mdahalo. Hata hivyo, amesema yeye ni mgombea, hivyo hatahudhuria, badala yake atatuma mwakilishi.

“Taarifa tunazo, mimi ni katibu mkuu lakini ni mgombea, niko kwenye ziara, nimemwomba Mwenyekiti Profesa Lipumba (Ibrahim) atuwakilishe na wakati ninamweleza aliridhia,” amesema Husna ambaye ni mgombea mwenza wa urais kupitia chama hicho.