Ahoua aendelea kuitesa Fountain, Sowah kama kawa

KINARA wa upachikaji mabao msimu uliopita, Jean Charles Ahoua ameendelea alipoishia kwa kuitesa Fountain Gate baada ya kufunga na kuasisti Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita Ahoua dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC, Simba ikiibuka na ushindi wa 4-0 alifunga bao moja na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao.

Mabao mengine katika mechi hiyo ambayo Fountain pia ilishindwa kutumia nyota wake kwa sababu ya kutokana na kutokamilisha usajili kama ilivyo msimu huu, yalifungwa na Edward Balua, Steven Mukwala na Valentine Mashaka.

Katika mechi ya leo iliyopigws kwenye Uwanja wa Mkapa,  kiungo huyo aliyetupia mabao 16 msimu uliopita aliasisti bao la kwanza kwa kupiga kona dakika ya tano,  iliyounganishwa kwa kichwa na beki Rushine De Reuck.


Licha ya Fountain Gate kuingia kinyonge na kushindwa kuendana na kasi ya mchezo, Elie Mokono hakutaka kuonyesha unyonge alijaribu mara kwa mara kulenga lango la Simba akiwa nje ya 18 na kuisaidia timu yake kuambulia kona moja dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Kona ya Fountain haikuwa na madhara langoni kwa Simba kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya Simba licha ya majaribio mengine ya mara kwa mara nje ya 18.

Ahoua alitumia dakika 37 kuifungia Simba bao la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa kiungo mkabaji Yusufu Kagoma na kukwamisha mpira nyavuni.

Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 45, huku Fountain Gate ikiambulia kuchonga kona moja hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga kuashiria mapumziko.


Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mzamiru Yassin na Kibu Denis nafasi zao zilichukuliwa na Morice Abraham na Alassane Kante mabadiliko ambayo yaliongeza burudani kwa mashabiki wachache waliojitokeza kwa Mkapa.

Mchezo ulikuwa unachezwa upande mmoja, huku Camara akisogea ndani kutoa maelekezo kwa wachezaji wenzake na dakika ya 57 Jonathan Sowah alishindilia msumari wa tatu akipokea krosi kutoka kwa Elie Mpanzu.


Simba walifanya mabadiliko tena wakimtoa De Reuck na kumuingiza Wilson Nangu, pia Shomari Kapombe alimpisha David Kameta na Kagoma alimpisha Neo Maema.

Licha ya kipindi cha pili Simba kuonyesha mpira mzuri kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi ilishindwa kutumia nafasi ilizozitengezeza kwa kuingia mara kwa mara langoni kwa Fountain iliyoshuka uwanjani na wachezaji 13 tu, wakiwamo 11 walioanza na wawili waliobaki benchi.

Ushindi huo umeifanya Simba kuwa timu ya pili kwa msimu huu kupata ushindi mnono ikiifuata Yanga iliyoshinda jana kwa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji, huku Azam ikifuata kwa kushinda 2-0 dhidi ya Mbeya City.

JKT Tanzania ndio vinara wa Ligi kwa sasa kwa tofauti ya mabao licha ya kulingana pointi na Mashujaa na Namungo kila moja ikiwa na nne baada ya kucheza mechi mbili mbili.