Mwanza. Chama cha Wataalamu wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT) kimesema kimeanza kutumia teknolojia ya akili mnemba (AI) katika utekelezaji wa majukumu yake.
Hata hivyo, kimesisitiza kuwa wataalamu wake hawawezi kupoteza ajira, bali wataendelea kuwa kiungo muhimu kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa ufanisi.
Akizungumza jijini Mwanza jana Septemba 25, 2025, katika kongamano la 38 la chama hicho lililofanyika sambamba na mkutano mkuu wa mwaka, Rais wa MeLSAT, Yahya Mnung’a, amesema wataalamu wa maabara hawapaswi kuwa na hofu ya kupoteza ajira kutokana na kuibuka kwa teknolojia mpya, kwani bado binadamu ndio watabaki mstari wa mbele katika kutoa huduma.
“Watumishi wa maabara ndio watakaoendesha mashine na kuhakikisha teknolojia hizi zinafanya kazi kwa usahihi. Tumekutana kujadiliana mbinu bora za kuendana na mabadiliko ya sayansi, ikiwamo matumizi ya akili mnemba ili kuboresha huduma,” amesema.
Amesema mashine za kisasa zinazotumia AI zina uwezo wa kufanya vipimo zaidi ya 3,000 kwa wakati mmoja na kuhudumia wagonjwa kati ya 50 hadi 100 kwa kutumia sampuli chache.
Hata hivyo, amesema bado kuna tafiti na kazi nyingi ambazo haziwezi kufanywa na mashine pekee, hivyo wataalamu wa maabara wanabaki kuwa kiungo muhimu katika mfumo wa afya.
Licha ya maendeleo hayo, amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi, akiitaka Serikali kuongeza ajira, hususani katika maeneo ya vijijini ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
“Idadi ya watumishi iliyopo bado haijakidhi mahitaji, hasa ikizingatiwa kuwa hospitali, zahanati na vituo vya afya vimewekewa vifaa vya kisasa vinavyohitaji wataalamu wa maabara,” amesema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Lebba amesema Serikali imejipanga kuhakikisha maabara zote nchini zinakidhi vigezo vya kutoa huduma, akionya kwamba maabara ambazo hazijasajiliwa au zitakazoshindwa kufuata taratibu zitafungwa mara moja ili kulinda usalama wa wagonjwa.
“Tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza. Wataalamu wa maabara tunawapa sampuli kupima, kisha tunalinganisha majibu yao na yetu ili kuhakikisha ubora wa huduma,” amesema.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema Serikali itaendelea kuimarisha kada ya maabara kutokana na nafasi yake nyeti katika sekta ya afya.
“Waajiri wanapaswa kutenga bajeti zitakazosaidia kutatua changamoto zinazoikabili taaluma ya maabara. Bila uchunguzi sahihi, matibabu hayatakuwa sahihi na jamii inaweza kudhoofika kiafya,” amesema.
Amesema maabara ni nyenzo muhimu ya kutoa huduma za afya na kwamba, ubora wa huduma unategemea ufanisi wa wataalamu waliopo.
Kutokana na hilo, amewataka wataalamu wa maabara kushirikiana na kuwa na mshikamano ili kukijenga chama chao na kufikia malengo waliyojiwekea.