Aziz KI aitamani Yanga, awataja Doumbia, Pacome

KIUNGO wa zamani wa Yanga aliyepo Wydad Casablanca ya Morocco, Stephane Aziz KI amesema mashabiki wa Jangwani wana kila sababu ya kunenepa msimu huu kupitia mastaa Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua.

Doumbia, raia wa Ivory Coast  ametua Yanga msimu huu akiwa mmoja wa nyota wa wanaoleta matumaini mapya ndani ya timu hiyo kutokana na ubora  wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz KI alisema mashabiki wa Yanga wana uhakika wa kufurahi kwa msimu mwingine kwa sababu ya wachezaji wawili makini ambao anawafahamu.

Alisema washambuliaji wa timu hiyo watanufaika na uwepo wa viungo  hao, kwani wana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kama zitatumika Yanga itafunga mabao mengi. “Naamini mashabiki wa Yanga wataendelea kufurahi kwa kuchukua mataji kutokana na uwepo wa Doumbia na Pacome kwa sababu nina uhakika umoja wao utakwenda kuwashangaza,” alisema.

“Doumbia kama ambavyo Ally Kamwe amempa jina la teknolojia ya AI ni kiungo hatari uwepo wake kucheza timu moja na Pacome hakuna timu itakuwa rahisi kutoka salama mbele ya Yanga.”

Aziz KI alisema wakati anapata dili la kuchezea Morocco aliacha jina la mchezaji huyo mezani kwa Hersi Said ili amsajili msimu huu haraka kutokana na ubora alionao.

“Doumbia akizoea ligi mtaona kitu tofauti kwani ni mtaalamu wa kutengeneza nafasi nina uhakika kina Prince Dube na Clement Mzize watafunga sana.”