Bolt Tanzania Yagawa Discount Inayoitwa “BOLTXSIMBU” Kusherehekea Medali ya Kwanza ya Dhahabu ya Tanzania.

Bolt Tanzania kwa fahari inatangaza kuzindua nambari mpya ya punguzo, SIMBU, kwa heshima ya Alphonce Felix Simbu, aliyefanya historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Riadha.

Ushindi wa Simbu umeiweka Tanzania kwenye ramani ya riadha ya kimataifa, sambamba na mataifa yenye nguvu kama Kenya. Huu si ushindi wa mtu binafsi pekee, bali ni alama ya kitaifa ya ubora na uwezekano. 

“Mwaka huu tuliahidi kujaribu tena, na limekuwa jambo kubwa. Nilishangazwa kwa sababu tulishindana na Wakenya, Waethiopia, na hata wao hawakuamini kuwa Mtanzania ameshinda,” aliwaambia waandishi wa habari alipowasili Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam jana, Septemba 23.

Ushindi wake unaleta ujumbe mzito kwa vijana wa Kitanzania kwamba kwa nidhamu na uvumilivu, wanariadha wengi zaidi wa dhahabu wataibuka kutoka nchini.

“Vipaji vinastahili kutambulika, na kama Bolt tunaona ushindi wa Simbu ni zaidi ya medali. Ni ushahidi kwamba vijana wa Tanzania wanaweza kupaa jukwaa la dunia na kung’aa,” alisema Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania na Kenya.

 “Kama vile Simbu alivyojizatiti kufanikisha ubora na kufika kwanza kwa kasi na usahihi, Bolt pia imejikita kuwasaidia Watanzania kusafiri kwa ufanisi, kwa gharama nafuu, na kwa wakati.”

Kwa mujibu wa Meneja wa Mahusiano ya Umma wa Bolt Tanzania, Gilbert Ginono, nambari hii maalum ya punguzo imezinduliwa kama njia ya kukuza chapa ya Simbu hapa nyumbani kufuatia ushindi wa kihistoria aliouleta. 

Kila safari inayowekwa kwa kutumia nambari hii si tu kusherehekea tukio la kitaifa la fahari, bali pia ni uthibitisho wa uwekezaji wa Bolt katika kutambua na kuinua vipaji vya Kitanzania.Kupitia mpango huu, Bolt inaendeleza dhamira yake ya kusimamia ufanisi, fursa na kusherehekea ubora — thamani zinazodhihirishwa na mbio za dhahabu za Simbu.