Tanga. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja ameahidi Serikali ya chama hicho itajenga nyumba bora kisha kuzikopesha kwa Watanzania masikini wasio na makazi.
Amesema hilo litasaidia kila mtu mwenye hali duni na asiye na makazi kuishi kwenye nyumba bora ambayo watakopeshwa kwa miaka 50 wakilipa kidogo kidogo.
Chama hicho kimesema haiwezekani hadi dunia ya leo bado kuna watu wanaishi kwenye nyumba za tembe na makuti.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 26, 2025 katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga wakati akiendelea na kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Tutajenga nyumba kwa Watanzania tuwakopeshe. Tunataka kila mtu aishi maisha mazuri. Tutawakopesha kwa miaka 50 walipe kidogo kidogo.
“Tunataka Chaumma tukafute nyumba za tembe, za nyasi na makuti. Haiwezekani toka tupate uhuru hadi leo watu waishi mwenye nyumba za namna hiyo wakati tuna kila rasilimali tulizopewa na Mungu, ikiwemo bahari mito na madini,” amesema.
Aidha, amesema Chaumma itarejesha mashamba ya mkonge Horohoro ili kuufanya uchumi wa eneo hilo la mpakani imara.
“Tuna mkakati wa kukufua mashamba ya mkonge, tuje na mbegu bora, tutatoa viatilifu na pembejeo kwa ajili ya mkonge. Watu walime kisasa, wapate ajira,” amezema.
Akifafanua zaidi amesema haiwezekani Watanzania walale kwenye makazi duni ya namna hiyo. Hivyo wapiga kura wawachague Chaumma waje na mkakati huo.
Mgombea mwenza huyo ameeleza mikakati ya kufufua uchumi wa Tanga kwa ujumla kwa kubinafsisha mashamba ya mkonge, ili watu walime, wakuze uchumi wao.

“Tanga ilikuwa na uchumi mkubwa, ilitambulika kwa sifa ya mkonge viwanda, tupeni Chaumma turejeshe heshima ya Tanga,” ameahidi.
Akitaja vipaumbele vyake, mgombea ubunge wa Jimbo la Mkinga, Rachel Sadick, jambo la kwanza amesema ardhi, fursa za vijana, madini ya mkinga kuwanufaisha wana mkinga.
Amesema atapigania suala la maji, huduma za afya, barabara, elimu, maji na umeme bila kusahau ajira, hivyo ameomba ridhaa kwa wananchi wampatie nafasi hiyo akawawakilishe vyema.
Chaumma inaahidi hayo wakati kampeni za urais, wabunge na madiwani zinaendelea kuchanja mbuga kote nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kwingineko, mgombea ubunge jimbo la Tanga Mjini, Zainab Ashraf akiongea katika kiwanja cha Makolola amesema jiji Tanga linahitaji kufufuliwa upya.
“Zinapita baiskeli hadi leo, hili ni jiji yanatakiwa yapishane magari. Tutakwenda kurudisha heshima ya jiji hili. Hapa kuna bandari, reli, kulikuwa na viwanda,” amesema.
Zainab amesema anaumizwa na hali ya kiuchumi ya jiji hilo akiahidi kurejesha uchumi kupitia viwanda kama ilivyokiwa zamani.
“Hatuna tena viwanda, mzunguko wa hela hakuna, tuna baiskeli mkitupa Chaumma, Tanga itainuka tena. Hiki ndio kipaumbele chetu.”