Dar es Salaam. Kutokana na kifo cha mgombea ubunge wa Fuoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abbas Ali Mwinyi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeahirisha uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo hadi pale itakapopanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea.
Abbas ambaye ni kaka mkubwa wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, alifariki dunia jana Septemba 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 25, 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Fuoni, Miraji Mwadini Haji, amepokea barua kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kuhusu taarifa ya kifo cha Abbas.
Amesema kutokana na kutokea kwa tukio hilo, uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Fuoni lililopo Wilaya ya Magharibi B- Zanzibar, umesitishwa kuanzia Septemba 25, 2025.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024, Tume kwa notisi itakayochapishwa katika gazeti la Serikali itapanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea na taratibu za uchaguzi wa ubunge katika jimbo husika zitaanza upya.
“Hivyo, uteuzi kwa wagombea wengine ambao walioteuliwa kihalali utabaki kama ulivyokuwa awali, isipokuwa kama mgombea atajitoa na kwamba hakutakuwa na kampeni kwa wagombea ubunge katika Jimbo la Fuoni mpaka baada ya uteuzi wa mgombea mwingine,” inaeleza taarifa hiyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi.