KMKM yaing’oa AS Port, yatinga raundi ya pili CAF

MABAHARIA wa visiwani Zanzibar, KMKM imekuwa timu ya kwanza ya Tanzania msimu huu kutinga raundi ya pili ya michuano ya kimataifa inayosimamiwa na CAF baada ya jioni hii kuifyatua kwa mara nyingine AS Port ya Djibouti kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja.

KMKM ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho Zanzibar na Ngao ya Jamii, imefuzu kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2 kwani katika mechi ya kwanza iliyopigwa pia uwanjani hapo wikiendi iliyopita, wenyeji wakiwa AS Port ilishinda pia 2-1.

Matokeo ya mechi ya ugenini iliwapa nguvu mabaharia hao ambao leo waliendelea kuonyesha wamepania kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza ya visiwani hapa kufika mbali katika michuano ya CAF ikitaka kurejea rekodi zilizowahi kuwekwa na Malindi miaka ya 1990.

Mechi ya jioni ya leo ulikuwa na ushindani mkali, huku pande zote zikionesha kiu ya kutaka kusonga mbele. KMKM walipata bao la kuongoza mapema kipindi cha kwanza, lililowekwa kimiani na nahodha Ahmed Is-haka ‘Babui’ dakika ya 43, lililodumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na wageni walijikuta wakimpoteza beki wa kati Mohammed Saleh dakika ya 61 na dakika kumi baadae wenyeji KMKM nayo ilimpoteza beki wa kati, Mohammed Mtumwa Hassan na kufanya kila moja kucheza na wachezaji 10.

Dakika ya 84 AS Port iliandika nao la kusawazisha, lakini dakika chache kabla ya kumalizika kwa pambano hilo KMKM iliongeza bao la pili na kuwahakikisha kutinga raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho ikisubiri mshindi wa mechi ya Jumapili kati ya Azam FC na El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini ambayo ilipoteza nyumbani wikiendi iliyopita kwa mabao 2-0.

Kocha wa KMKM, Hababuu Ali alisifia nidhamu ya wachezaji wake, akisema kuwa ushindi huu ni matokeo ya maandalizi mazuri na mshikamano wa timu.

“Hii ni hatua muhimu, lakini bado safari ni ndefu. Tunahitaji kuongeza nguvu na kujiandaa vyema kwa raundi ijayo,” alisema Hababuu.

Mbali na KMKM, timu nyingine zilizotinga raundi hiyo ya pili ya Kombe la Shirikisho jioni hii ni, Ferroviario Maputo ya Msumbiji iliyoitoa AS Fanalamanga ya Madagascar pamoja Royal Leopards Eswatini iliyoing’oa Young Africans ya Namibia kwa jumla ya mabao 7-0.