Matapeli 260 wa Kimapenzi Mtandaoni, Wakamatwa Afrika – Global Publishers



Mamlaka katika nchi 14 barani Afrika zimewakamata watu 260 katika msako mkubwa dhidi ya uhalifu wa kimtandao unaohusisha utapeli wa kimapenzi. Operesheni hiyo, iliyofahamika kama Operation Contender 3.0, iliongozwa na INTERPOL kati ya Julai 28 na Agosti 11, 2025.

Katika oparesheni hiyo, zaidi ya vifaa vya kielektroniki 1,200 vilikamatwa, Vituo 81 vya uhalifu mtandaoni ilifungwa, na karibu waathiriwa 1,500 walitambuliwa kote barani. Hasara inayokadiriwa kutokana na matapeli hao imefikia dola milioni 2.8 (takribani shilingi bilioni 7 za Kitanzania).

Matapeli walitumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kuchumbiana mtandaoni kuwadanganya waathiriwa. Katika utapeli wa kimapenzi, walitengeneza akaunti bandia zenye picha zilizoporwa, huku kwenye visa vya “sextortion,” waathiriwa walilazimishwa kutoa fedha baada ya kurekodiwa au kutishiwa kusambaziwa picha na video za faragha.

Waathiriwa wakubwa mara nyingi ni watu wanaotafuta uhusiano wa kimapenzi mtandaoni, hasa wale wenye upweke au matatizo ya kifamilia. Vijana pia wanajikuta wakihangaika pale wanapodanganywa kutuma picha au video za faragha ambazo baadaye zinageuzwa silaha ya kuwabana.

Kwa baadhi ya vijana barani Afrika, hasa wale wasio na ajira, utapeli huu umegeuka kuwa “kazi ya haraka ya kupata fedha.” Kutengeneza akaunti bandia na kuwalaghai watu mtandaoni kumechukuliwa kama chanzo cha mapato, jambo linaloongeza kasi ya kuenea kwa uhalifu huu.