Njombe. Mgombea ubunge wa Njombe Mjini kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Sigrada Mligo amesema endapo atachaguliwa atahakikisha anapambania mabadiliko ya sheria ya kodi ya mazao ya kilimo kwa kuwa tozo na ushuru imekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima na wafanyabiashara mkoani Njombe.
Mligo ametoa kauli hiyo leo Septemba 26, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital katika kipindi hiki cha kampeni ya wagombea wa nafasi mbalimbali kupitia mahojiano maalumu yaliyofanyika Njombe.
Amesema wakulima na wafanyabiashara wanakumbana na tozo hizo hasa kwenye mageti wakati wa kusafirisha mazao kwa ajili ya kwenda kutafuta masoko kwenye mikoa mingine nchini.
“Njiani humu kuna mageti na ukipita lazima usimamishwe, ukaguliwe na endapo umezidisha mzigo hata kidogo tu, faini yake ni Sh300,000 mpaka Sh2 milioni,” amesema Sigrada.
Amesema mtu wa aina hiyo akipigwa faini ya namna hiyo hawezi tena kufika kwa wakulima kwa ajili ya kununua mazao kwa gharama za awali kwa kuwa haiwezi kumlipa hasa akifikiria changamoto katika mageti.
Ameongeza kuwa mpaka sasa kupitia chama chao, wamepita katika kata saba kati ya 13 za jimbo la Njombe na kampeni bado zinaendelea na wamekuwa wakipokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Amesema kila siku wana ratiba ya kwenda kwenye kata na vijiji lakini kupitia hizo kampeni wanakutana na vitu vingi kwanza wananchi wamechoka na wana maisha magumu kiasi cha kushindwa kununua hata mafuta ya kupaka.
“Mkulima amelima viazi na gunia linauzwa Sh15,000 lakini hata wakununua hayupo, wewe uliyepanda unambembeleza mnunuzi,” amesema Sigrada.
Mgombea huyo amesema kuna viazi vililimwa tangu Desemba 2024 huko vijijini, vinaitwa “mabibi” mpaka sasa, vipi shambani havina mnunuzi na unakuta mkulima katumia gharama kubwa katika kilimo.
Amesema watu wamekata tamaa ya kupiga kura kwakuwa hata mpinzani akishinda hawezi kutangazwa na mamlaka kutokana na mfumo uliopo sasa ambao umekuwa siyo rafiki kwa vyama vya upinzani.
“Wananchi wanasema wanapenda kupiga kura lakini mmejipangaje kulinda hizo kura kwa sababu hata mkishinda hamuwezi kutangazwa,” amesema Sigrada.
Amesema wananchi wamepoteza imani na kuona uchaguzi haupo kwa ajili ya kupata viongozi watakaowawakilisha bali umegeuka kuwa sehemu ya watu wachache kujinufaisha.
Amesema wananchi huko vijijini wamebakia kunywa pombe kuanzia asubuhi siyo kwasababu wanapenda bali ni matokeo ya kukata tamaa kulingana na hali ya ugumu wa maisha ilivyo.
Mgombea udiwani Kata ya Uwemba kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Jactan Mtewele amesema mwitikio wa wananchi katika kushiriki kampeni ni mzuri kwa kuwa wanaona yaliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano lakini msisitizo wao ni kukamilisha yale ambayo bado.
Amesema katika kampeni ambazo anaendelea kufanya kilio kikubwa cha wananchi kwenye kata hiyo ili mahitaji ya barabara pamoja na maji ambapo changamoto hizo zikitatuliwa hakuna maneno mengine.
“Sisi tunashukuru mwitikio ni mzuri na watu kwa kweli Oktoba wanakwenda kutiki kwa mheshimiwa Rais, mbunge na diwani wa kata husika,” amesema Mtewele.
Nao baadhi ya wananchi mkoani humo, akiwemo Gwakisa Mwakanyamale, amesema kampeni za mwaka huu zimeegemea upande mmoja wa CCM kwani tangu amefika hajaona shamrashamra kutoka katika vyama vingine.
“Mwamko wa wananchi kushiriki kampeni upo lakini siyo kama miaka iliyopita na nadhani sababu ni vyama vya upinzani vilivyopo havina nguvu,” amesema Mwakanyamale.
Kwa upande wake, Joseph Mligo amesema mikutano kama haipo na kama inafanyika ni kimaficho na hiyo huenda inasababishwa na wananchi kupoteza matumaini kutokana na kukosekana kwa vyama vya upinzani vyenye nguvu.
“Ushindani hakuna tofauti na miaka ya nyuma ulikuwa ukienda kwenye chama hiki unaondoka na hili na chama kingine onaondoka na lile,” amesema Mligo.