Na Said Mwishehe,Lindi
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo Serikali itakwenda kujenga majosho na machinjio bora kwa mifugo ili nyama ya Tanzania iwe yenye viwango kutambulika maeneo mbalimbali duniani.
Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuchukua katika sekta ya mifugo nchini na miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele ni Serikali kutoa ruzuku ya chanjo ya mifugo.
Kwa upande wa mifugo katika maeneo ya Kitomanga na Mipingo katika Jimbo la Mchinga amesema alieleza ruzuku ya chanjo kwa mifugo itatolewa.
“Kwenye ruzuku ya chanjo siyo Kitomanga na Mipingo peke yake. Maeneo yote yenye ng’ombe tumesema tutatoa ruzuku ya chanjo. Kama chanjo inalipiwa sh. 20,000 mfugaji atalipia sh. 10,000. Kama ni sh. 30,000 mfugaji atatoa 15,000 na serikali itamalizia.
“Kwa upande wa kuku, chanjo zote ni bure. Twende tukachanje mifugo yetu kwani madhumuni ya kuchanja ni kwamba kwa muda mrefu tulikuwa tukihangaika kutafuta soko.
Aliongeza: “Tanzania hatukuwepo kwenye orodha ya nchi zinazochanja mifugo kwa hiyo afya ya mifugo yetu haikuwa ikitambulika. Tumetoa ruzuku ya chanjo ili mifugo yote ya Tanzania itambulike na tuweze kuingia katika soko la kimataifa.”
Pia amesema mbali na chanjo serikali itakwenda kujenga majosho na machinjio bora kwa mifugo ili nyama ya Tanzania iwe yenye viwango kutambulika maeneo mbalimbali duniani.
Kuhusu uvuvi, Mgombea Urais Dk.Samia amesema kwamba serikali ilitoa mikopo ya boti za kisasa za uvuvi zenye thamani ya Sh.milioni 712 huku awamu ijayo serikali itaendelea kutoa boti na vifaa vya uvuvi.
Pia amesema katika maeneo ya Mkoa wa Lindi huduma zote za afya zinapatikana zikiwemo za kibingwa baada ya uwepo wa hospitali kubwa ya rufaa.”Kwa bahati nzuri jirani zenu wa Mtwara wanapata huduma za kibingwa kwa hiyo kwa ukanda wa kusini masuala ya afya yapo vizuri sana. Tutaendelea na kasi ileile.”
Akizungumza kuhusu elimu amesema kwamba endapo akipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, serikali yake itajikita zaido kujenga nyumba za walimu.
“Mchinga ni eneo lililochaguliwa kuwa na shule maalum ya mchepuo wa sayansi kwa wasichana. Changamoto ndogo walizokuwa nazo tumeziondoa kwa huyo matumaini yangu kwamba wataendelea kusoma vizuri.
“Serikali imeanzisha shule ya ufundi stadi Dk. Jakaya Kikwete iliyopo Kata ya Nangaro ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 70.Ujenzi huo utakamilika kuwezesha vijana wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.Hiyo ndiyo CCM, hatusemi kutoka ndotoni. Tukisema tunatekeleza,”amesema Dk.Samia.
Kuhusu umeme, ameeleza vitongoji vilivyosalia kufikishiwa huduma hiyo wakandarasi wanaendelea na kazi ikiwa ni utekelezaji ajenda ya nishati safi.
“Vitongoji vyote vitakapopata umeme, matumizi ya kuni yatapungua.Tutatumia gesi au umeme kufanya mapishi yetu na tuiache misitu ipumue kidogo ili hali yake irejee ndani ya nchi yetu. Tutandelea na kasi ileile.
“Pia Serikali inatambua mahitaji ya miundombinu ikiwemo ukarabati wa barabara hivyo aliwaahidi maboresho ya barabara zilizoainishwa katika ilani ya uchaguzi.