KOCHA wa zamani Yanga, Miloud Hamdi ana hali mbaya huko Misri kutokana na timu anayoinoa ya Ismalia kufanya vibaya katika Ligi Kuu nchini humo, lakini hilo halijamzuia kufuatili kinachoendelea Msimbazi baada ya Simba kukimbiwa na Kocha Fadlu Davids.
Hamdi aliyeiongoza Ismalia katika mechi nane na kushinda moja kutoka sare moja na kupoteza sita, timu hiyo ikifunga bao moja tu na kufungwa tisa, ikiburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 21 kwa sasa hatua hii ya awali, alisema kocha mpya atakayetua Simba atakuwa na kibarua kizito.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Singida Black Stars kabla ya kutua Yanga, alisema kocha mpya atakayetua Simba atakuwa na kazi kwa vile timu bado iko katika presha kama ilivyokuwa kwake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema kwa mtazamo wake ananaona ulikuwa muda sahihi kwa kocha Fadlu kuondoka, kwani hawezi kupinga uamuzi ya mtu binafsi licha ya wengi kuona amekosea hasa ikizingatiwa amesajili timu hiyo na kuanza nayo maandalizi ya msimu mpya.
Alisema Fadlu ni moja kati ya kocha bora aliowahi kukutana nao na ameifanyia Simba mambo maengi makubwa, ila shida ni kutokuweka rekodi ya kuifunga Yanga na kuchukua ubingwa, jambo ambalo kwa hizo timu kubwa mbili ndio kipimo cha kazi ya kocha na kuchangia presha kubwa.
“Nimesikia Fadlu ameenda Raja, hii haiwezi kuwa taarifa nzuri kwa mashabiki lakini ndivyo maisha ya ukocha yalivyo. Wakiwa pre season, nilikuwa naenda kumsalimia kambini, ni kocha mzuri, lakini kitu kizuri amewaachia Simba, alitengeneza timu nzuri ambayo kama watapata kocha mwenye utulivu atakayeweza kuwaunganisha wachezaji itakuwa hatua kubwa,” alisema Hamdi ambaye aliweka rekodi ya kuchukua mataji matatu akiwa na Yanga ikiwamo Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na Muungano kabla ya kunyakuliwa na Ismalia na mambo hadi sasa kumwendea kombo.
Hamdi alisema, licha ya kikosi kipana ilichonacho Simba, lakini anaona kuondoka kwa Fadlu kutawapa tabu wachezaji kisaikolojia na hivyo kocha yeyote atakayeajiriwa atakuwa na kazi kubwa kuwarudisha katika mstari na kurejesha morali ya zamani.
“Wasiwasi wangu wasipate kocha ambaye atakuwa na falsafa tofauti zaidi na zile za kocha aliyetoka hapo watapata shida, ujue sisi licha ya kufundisha soka lenye sheria moja ila kila mtu ana mbinu zake,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Angalia nikiwa Singida, lakini nilipofika Yanga, nilikuta falsafa zao zilikuwa hazitofautiani sana na zile zangu, niliamua kuacha kwanza ili nisiwachanganye wachezaji, nikawa naingiza vitu vichache sana taratibu na mwisho tulifanikiwa, hiyo akili akiwa nayo aliyemrithi Fadlu basi Simba itakuwa salama sana.”