Mpemba alivyomuua mkewe, kumzika chumbani

Morogoro. Wivu wa mapenzi ni jinamizi linalotafuna roho za wapendanao, kauli inayoshabihiana na kilichotokea kwa Mohamed Salahange maarufu Mpemba, aliyemuua mkewe, kisha kuuzika mwili chumbani kwao.

Baada ya kuuzika mwili huo, akiwatuma watoto wa mama huyo kuleta mchanga chumbani bila kujua ni kwa ajili ya kumzika mama yao, walihama nyumba na kuifunga hadi siku 81 mwili huo ulipofukuliwa chumbani.

Hii ni baada ya Mpemba kuwatisha watoto wa marehemu ambao alizaa na mwanamume mwingine kabla ya kumuoa, kuwa wasiseme lolote kwa kuwa chochote watakachofanya au kusema, yeye atakisikia hata kama hayupo nao.

Lakini ushahidi wa mmoja wa watoto hao, Moreen Shoo (13) ambaye siku ya tukio alipigwa kwa rungu na baba yake huyo wa kambo na kufungiwa katika chumba kimojawapo, alisimulia kila kilichoendelea hadi mauaji ya mama yake.

Simulizi ya mauaji hayo imo katika hukumu ya Jaji Khadija Kinyaka wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, aliyoitoa Septemba 22, 2025. Hukumu hiyo imepakiwa kwenye tovuti ya Mahakama leo Septemba 26, 2025.

Mohamed Omary Salange, akitoka Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Morogoro,  baada ya kuhukumiwa jena miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kike wa kufikia. Picha na Johnson James



Jaji Kinyaka amemtia hatiani Mpemba kwa kosa la kumuua mkewe kwa kukusudia na kumhukumu kunyongwa hadi kufa, akisema hiyo ndiyo adhabu pekee inayotamkwa na sheria kwa kosa la kuua kwa kukusudia.

Kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka, mauaji ya Beatrice Mgongolwa yalitokea Januari mosi, 2024 huko Kimamba A, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, lakini mwili wake ulifukuliwa Machi 22, 2024, ikiwa siku 81 zimepita.

Moreen, aliyekuwa shahidi wa sita wa upande wa mashitaka, anasimulia  Januari mosi, 2024 kulitokea ugomvi kati ya baba (Mpemba) na mama (Beatrice), uliohusiana na wivu wa mapenzi wa baba yao.

Siku hiyo, Mpemba alimtuhumu mama yake kuwa aliingiza mwanamume mwingine chumbani kwao na kulingana na maelezo ya baba ni kuwa kuna alama aliziacha katika eneo la kuingia chumbani na aliporudi alikuta hazipo.

“Siku hiyo, baba aliondoka asubuhi na kurudi saa 4:00 asubuhi. Aliporudi alimwita mama na kumwambia ni lazima alikuwa na mwanamume mwingine kwa sababu alama alizokuwa ameweka hazipo,” alisimulia Moreen katika ushahidi wake.

Alisema: “Mama yetu alisema hakuna mwanamume aliyeingia na kwamba alikuwa amenituma mimi kufagia chini. Baba alimchukua mama hadi chumbani kwao na kuanza kumpiga. Wakati mama anapigwa nilikuwepo ndani ya nyumba.”

“Mimi pia nilipigwa pamoja na mama ndani ya chumba cha baba na mama. Baba alisema watoto wa kike wanajua siri za mama zao. Wadogo zangu walikuwa nje na walifungiwa huko nje ili waangalie kuku,” alisema na kuongeza:

“Baba alikuwa anatupiga kwa kutumia rungu, jembe na panga. Nilipoingilia kumkinga mama, alinipiga na rungu kichwani na maeneo mengine. Baadaye alinitoa chumbani kwao na kwenda kunifungia chumbani kwangu.”

Anaeleza: “Alirudi chumbani kwao na kuendelea kumpiga mama. Nilimsikia baba akimwambia mama nitakupiga hadi ufe. Nilimsikia mama akilia kwa maumivu. Alimchukua mama na kumleta sebuleni. Nilimsikia akimburuza.”

“Mama alikuwa anaomba maji ya kunywa lakini baba akamwambia siwezi kukupa maji ili asije akaenda kusimulia huko ahera kuwa alimpa maji. Baba alimwambia mama usilie kama kondoo. Akamwambia usinipakaze damu zako,” anaeleza na kuongeza:

 Mohamed Salange (37) (mwenye pingu) akipelekwa jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Hakimu Mkazi,  Lameck Mwamkoa. Picha na Johnson James



“Akamwambia mama asubiri ili akachukue panga ammalize. Nilisikia kishindo cha pigo moja ambalo sikujua ni pigo la nini nilisikia sauti ya kipigo kisha sauti ya kukoroma. Mkoromo ulikuwa unatoka sebuleni. Baadaye, sikusikia chochote.”

Moreen alieleza alisikia kitu kinaburuzwa kutoka sebuleni kuelekea chumbani kwa wazazi wake na kufuatiwa na sauti ya kuchimba ardhini kisha alimfungulia na kumwagiza yeye na wadogo zake kwenda kuleta mchanga.

Walipoingia ndani ya chumba cha wazazi wao walikuta kuna eneo liko kama kaburi, siku iliyofuata baba yao aliondoka na aliporudi jioni aliwaambia mama yao ametoroka na wasije kumwambia mtu yeyote kuhusu suala hilo.

Ushahidi wa mashahidi wengine ulieleza baada ya mkewe kutoweka, Mpemba aliendelea kukaa katika nyumba yake kwa siku chache kisha alihama yeye na familia yake na kwenda kuishi Ludewa kwa shahidi wa tatu, Josephina Madole.

Kutoweka kwa mama yake na maelezo ya baba yao kulimtatiza Moreen siku hadi siku, ndipo siku moja alimsimulia kila kitu shahidi wa tatu, ambaye alimchukua pamoja na wadogo zake na kuwapeleka Kituo cha Polisi Kimamba.

Wakati hayo yakitokea, Mpemba alikuwa mahabusu akishikiliwa na Polisi kwa kosa la kumtapeli mpenzi wake wa zamani aitwaye Angela.

Baada ya Polisi kusikiliza imulizi hiyo, walikwenda kwenye nyumbani ya mshitakiwa ambayo alihama wakaizungushia utepe. Machi 21, 2024 taarifa zilifikishwa Idara ya Upelelezi ya makao makuu ya Polisi Morogoro.

Mohamed Omary Salange, akitoka Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Morogoro,  baada ya kuhukumiwa jena miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kike wa kufikia. Picha na Johnson James



Siku iliyofuata, timu ya makachero, daktari na mshitakiwa walikwenda hadi eneo la tukio ambako mshtakiwa ndiye aliwaongoza hadi sehemu alipokuwa amemzika mkewe na mwili ulifukuliwa na kutambuliwa ni wa Beatrice.

Katika utetezi wake, mshitakiwa aliyekuwa akitetewa na wakili Anna Ndahani, alikana kumuua mkewe na kueleza kifo chake kilisababishwa na mwanamume mwingine ambaye alimpiga Beatrice na kitu asichokijua.

Mpemba katika kujinasua, alieleza mwanamume huyo alikirusha kitu hicho kumpiga yeye kutokana na ugomvi baina yao baada ya yeye (Mpemba) kumfumania mkewe akifanya mapenzi na mwanamume huyo Machi 20, 2024.

Aliiambia mahakama kuwa mkewe alipigwa na kitu hicho na kuanguka chini na alijaribu kumuamsha bila mafanikio na kwamba, alipogundua mkewe haamki, alikaa chini na kuanza kulia na kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kimamba.

Baada ya kufika kituoni, aliwekwa chini ya ulinzi na alipoulizwa kuhusu Januari mosi, 2024 kuwa ndiyo siku ya mauaji, alisema tarehe hiyo alisherehekea mwaka mpya na familia yake na hakuna kitu kibaya kilitokea.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa na kuuchambua kwa kina, Jaji Kinyaka amesema upande wa mashitaka umethibitisha shtaka pasipo kuacha shaka yoyote kuwa ndiye muuaji.

Jaji amesema ushahidi wa shahidi wa sita, Moreen ambaye alishuhudia kile kilichofanyika, ulikuwa mzito na uliunganika na wa mashahidi wengine, akiwamo wa tano, Victoria Mnyambeyu ambaye ni jirani yao.

Katika ushahidi wake, Victoria alieleza namna siku ya tukio alivyosikia sauti ya mwanamke akilia kutoka katika nyumba ya mshtakiwa na kwamba, kabla ya siku hiyo, mshtakiwa aliwahi kumpiga mkewe.

Jaji amesema ushahidi wa kupatikana kwa mwili ukiwa umezikwa ndani ya chumba walichokuwa wakilala baada ya kufukuliwa, unamuunganisha moja kwa moja mshtakiwa na mauaji hayo na ni yeye mwenye alionyesha alipomzika.

“Kitendo cha mshitakiwa kutotoa taarifa kwa polisi juu ya kupotea kwa mkewe kinaacha maswali mengi. Yeye ndiye mtu mzima na wanafamilia wengine ni watoto, ndiye alitarajiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa na Polisi,” amesema na kuongeza:

“Lakini hakufanya hivyo hadi shahidi wa tatu, Josephina, wa sita Moreen na wadogo zake walipofika polisi na kueleza mkasa wote na mshtakiwa mwenyewe kuongoza timu ya makachero hadi mahali alipomzika mkewe.”

Jaji ameukataa utetezi wa mshtakiwa kuwa mkewe alipigwa na kitu na mwanamume mwingine na kwamba, mwili wake ulikutwa sebuleni na siyo chumbani ukiwa umezikwa kuwa ushahidi huo haujautikisa hata chembe ushahidi wa Jamhuri.

Kwa mujibu wa Jaji, mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kutenda kosa hilo kutokana na aina ya silaha alizozitumia, nguvu aliyoitumia kumpiga, maeneo aliyompiga ambayo ni pamoja na kichwani na kitendo cha kuuzika mwili wake.

Ni kutokana na uzito wa ushahidi huo, Jaji amemtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.