Mbeya. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi akichaguliwa kushika wadhifa huo atapandisha bei ya mazao ya viazi na pareto sokoni ili kuongeza kipato cha wakulima na kuinua uchumi wa wananchi wa Mbeya na maeneo mengine ya kilimo nchini.
Pia, ameahidi kujenga barabara ya Mbalizi- Shigamba kwa kiwango cha lami, ikiwa ni utekelezaji wa sera iliyopo kwenye ilani ya chama hicho ya kujenga miundombinu kuanzia maeneo ya uzalishaji ili kuzalisha ajira na matajiri.
Kwa sasa, zao la pareto wakulima wanauza Sh45,00 kwa kilomoja, lakini nje ya nchi kama Kenya, kiasi kama hicho kinauzwa Sh25,000 kwa thamani ya fedha ya Kitanzania, Wakati gunia moja la viazi wakulima hao wanauza Sh22,000.
Akihutubia Leo Septemba 25, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Itizi, Kata ya Santilia, mkoani Mbeya, Mwalimu amesema mfumo wa sasa wa masoko unawanyonya wakulima kwa kuwalipa bei ya chini, huku walanguzi wakipata faida kubwa katika soko la kimataifa.
“Kilo moja ya pareto inauzwa Sh4,500 hapa nyumbani, lakini inauzwa hadi Sh25,000 nje ya nchi. Hii ni dhuluma. Kama mtaendelea kuikumbatia CCM, mtaendelea kuwa maskini,” amesema.
Mwalimu ameeleza serikali ya Chaumma itajenga mfumo wa haki wa bei kwa mazao ya kilimo na kuhakikisha wakulima wanapata faida halali ya jasho lao.
Amesema lengo ni kuhakikisha pareto inaweza kuuzwa hadi Sh20,000 kwa kilo sokoni, hatua itakayoongeza kipato cha wakulima na kuchochea uchumi wa maeneo ya kilimo kama Mbeya.
“Viazi vyenu vinachukuliwa na Wakenya, wanaenda kuuza Ulaya na kutajirika, wakati nyie mnabaki maskini,” amesema.
Katika kuboresha mazingira ya uzalishaji, mgombea huyo pia ameahidi ujenzi wa barabara ya lami ya Mbalizi–Shigamba na kuunganisha maeneo ya kilimo kama Ilembo hadi Mbeya ili kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo.
“Najua nikijenga barabara, mtasafirisha mazao kwa gharama ya chini, lakini pia pembejeo zitawafikia kwa wakati,” amesema.
Akiangazia ajira kwa vijana, Mwalimu amesema serikali ya Chaumma itaweka mkazo katika kuwaunganisha wakulima na masoko ya kimataifa, kuongeza thamani ya mazao, na kutoa ajira kupitia kilimo chenye tija.
Kwa upande wake, Rajo Mlojoe, mgombea udiwani Kata ya Santilia kupitia chama hicho, amesema sababu kuu ya kuwania nafasi hiyo ni kushindwa kwa waliowahi kuwa wawakilishi wa wananchi kukidhi matarajio ya wanachi.
Ameeleza kuwa changamoto kuu zinazoikumba Kata ya Santilia ni pamoja na miundombinu duni ya barabara, uhaba wa walimu, na mazingira duni ya kazi kwa walimu waliopo.
“Changamoto moto yetu ni miundombinu ya barabara katika Kata yetu ya Santilia pamoja na Kata jirani. Lakini jambo lingine kubwa ni uhaba wa walimu. Hata waliopo hawana makazi bora,” amesema Mlojoe.
Kwa mujibu wa Mlojoe, Kata ya Santilia ina jumla ya wakazi wapatao 16,000, hali inayohitaji utaratibu mpya wa kiutawala ili kuboresha utoaji wa huduma.
“Ili kuufanya utawala uwe rafiki kwa wananchi, Kata hii inapaswa kugawanywa. Idadi ya watu ni kubwa mno kwa kata moja, jambo linalolemaza huduma za kijamii,” amesema.
Mbali na hayo, Mlojoe amegusia tatizo la maji safi na salama, pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana ambao licha ya kumaliza vyuo, wamelazimika kubaki majumbani bila ajira.
“Tuna changamoto ya maji. Vijana wengi wamehitimu vyuo, lakini hawana kazi ya kufanya. Wamekuwa mzigo kwa familia, hali inayozua msongo na kukatisha tamaa,” amesema.