LIGI ya Kikapu Dar es Salaam (BDL) inazidi kunoga ikiwa ni hatua ya nusu fainali na timu zinacheza michezo mitatu ‘best of three pray off’ kujitafutia nafasi ya kutinga fainali, kwenye Uwanja wa Donbosco Oyster Bay, Upanga, jijini Dar es Salaa.
Mchezo wa JKT dhidi ya Pazi ulishuhudiwa wapinzania hao wakigawana ushindi katika michezo miwili ya mwanzo baada ya kila moja kushinda. JKT ndiyo ilikuwa ya kwanza kushinda kwa pointi 80-54, kabla ya Pazi kushinda 66-52 na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Ikiwa na kikosi chao kamili, Soro Geofrey, Ethan Jamego, Victor Michael na Robert Tasire Pazi iliibana JKT ikisaka kulipa kisasi katika robo ya kwanza na kuwafanya wapinzani wao hao washindwe kupenya eneo lao na kuongoza kwa pointi 22-14.
Hata hivyo, iliibidi JKT kubadili mbinu na kuamua kufunga kwa mtupo mmoja wa pointi tatu na kuongoza kwa 20-12, kabla pazi haijapindua meza na kuongoza kwa pointi 17-9, 10-9.
Ethani Jamego aliongoza kwa kufunga pointi 16, akifuatiwa na Victor Michael aliyefunga 12, huku akiongoza kwa kudaka mipira ya rebound mara sita na kwa JKT, Omari Sadiki alifunga pointi 15 akifuatiwa na Jackson Brown aliyefunga 11.
Baada ya kichapo hicho, nyota wa Pazi Victor Joseph alisema makosa waliyoyafanya katika mchezo huo walirekebisha baada ya kukutana mazoezini.
“Kwa kweli siku ya kwanza tulicheza kiwango cha chini tofauti na michezo mingine tuliyowahi kucheza katika Ligi ya BDL,” alisema Michael na kuongeza ushindi walioupata umeongeza chachu ya wao kufanya vizuri katika mchezo unaofuata uliopigwa jana Alhamisi usiku na mshindi ataingia fainali akiongoza kwa michezo 2-1.
Kwa upande wa wanawake, JKT Stars tayari imetinga fainali baada ya kuifungwa DB Troncatti katika michezo 2-0.

JKT iliyomaliza michezo 15 ya mzunguko kwanza bila kupoteza hata mmoja imeendeleza ubabe wake hadi kutinga fainali ikiwa ni timu pekee ambayo haijafungwa na katika mchezo wa kwanza nusu fainali, ilishinda kwa pointi 75-48 na wa pili 61-46.
Katika nusu fainali ya pili, DB Troncatti ilianza mchezo katika robo ya kwanza kwa kasi, huku JKT Stars ikiusoma mchezo na ikiwa chini ya kocha mzoefu, Esther Nelson akisaidiwa na Lulu Joseph, ilidhihirisha ubora wao.
DB Troncatti iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 18-17, robo ya pili JKT Stars ikaongoza kwa pointi 15-11,10-10, 19-7.
Katika mchezo huo Jesca aliongoza kwa kufunga pointi 25, akifuatiwa na Sara Budodi 13 akiongoza pia kwa udakaji wa mipira (rebound) mara nane na assisti alitoa sita na upande wa timu ya DB Troncatti alikuwa Jesa Lenga aliyefunga pointi 20.
Hata hivyo, licha DB Troncatti kupoteza mchezo huo, ilionyesha kiwango kizuri ikiongozwa na Jesca Lenga, Irene Gerwin na Nasra Bakari.

Kutokana na ubora wa ligi hii, imejumuisha pia waamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha michezo ya nusu fainali na fainali, huku wenyewe wakiisifia pamoja na wachezaji.
Waamuzi hao ni Justus Akhwesa, Francis Ochieng (Kenya) na Liliana Bagnata (Msumbuji), wanashirikiana na mwamuzi wa mzawa, Shaban Mahobony
Akhweza alisema anajisikia furaha kuchezesha ligi ngumu ya BDL.
“Kwa kweli nimeona wachezaji wamekuwa wakiheshimu mahamuzi nayotoa uwanjani.”
Akiongea na Mwanaspoti katika uwanja wa Donbosco Oysterbay kocha wa kikapu kutoka Temeke Ally Issa alipongeza uongozi wa BD kwa kuleta waamuzi wa kimataifa kuchezesha nusu fainali pamoja na fainali.
“Kwa kweli waamuzi hawa wanachezesha kwa kufuata sheria na kanuni za uchezeshaji, sijasikia lawama zozote kutoka kwa mashabiki,” alisema Issa.

Baada ya kutokufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu, Kurasini Heat imeanza maandalizi mapema kwa ajili ya msimu ujao, ikiwamo kusaka wawekezaji watakaoisimamia na kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa.
Akiongea na Mwanasposti katika viwanja hivyo, kiongozi wa timu hiyo, Mussa Kago alisema wameamua kufanya hivyo ili kutengeneza timu itakayotoa ushindani mwakani.
“Unajua timu bila ya kuwa na mwekezaji huwezi kufanya chochote, kwa upande wetu tumejipanga mimi na viongozi wenzangu kutafuta mwekezaji,” alisema Kago.
Akizungumzia kuhusu ligi ya mwaka huu, alikiri timu yake haikuwa na maandalizi mazuri na ilishika nafasi ya 13, katika msimamo kwa pointi 19.
Timu hiyo ambayo ilipanda daraja pamoja na Stein Warriors na Polisi iliwahi kuwa bingwa wa ligi hiyo mwaka 2020 baada kuifunga JKT katika fainali kwa michezo 3-1.