Dar es Salaam. Mjane, Alice Haule amewasilisha maombi ya kufungua shauri la madai ya ardhi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, sambamba na maombi madogo, akiomba zuio la muda la kutoondolewa kwenye nyumba.
Alice na mfanyabiashara Mohamed Mustafa Yusufali, wana mgogoro wa umiliki wa nyumba iliyopo kiwanja namba 819, chenye hati namba 49298, Msasani Beach, Dar es Salaam.
Kutokana na mgogoro huo, Septemba 23, 2025 mali za wapangaji wa Alice ziliondolewa kwa nguvu kwenye nyumba hiyo, tukio lililosababisha Jeshi la Polisi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuingilia kati.
Katika maombi ya kufungua shauri la madai ya ardhi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, wajibu maombi ni Yusufali, Msajili wa Hati na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika shauri hilo namba 24396/2025, Alice anaiomba mahakama itamke kuwa uhamishaji wa hati ya miliki ya nyumba hiyo kwenda kwa Yusufali kutoka kwa mume wake, Justice Rugaibula (sasa marehemu) ni wa udanganyifu, hivyo ni batili.
Badala yake anaiomba mahakama itamke kuwa nyumba hiyo ni mali ya Rugaibula na itoe amri ya kubatilisha uhamishaji umiliki wa nyumba kutoka jina la Rugaibula kwenda kwa Yusufali.
Vilevile, anaiomba mahakama imuamuru Yusufali amlipe Sh200 milioni kama fidia ya madhara ya jumla, pamoja na gharama za kesi.
Kwa mujibu wa nyaraka za shauri hilo, pamoja na kiapo cha Alice kinachounga mkono shauri dogo la maombi ya zuio, ambazo Mwanachi limeziona, anadai hapajawahi kuwepo makubaliano ya kumuuzia nyumba Yusufali.
Badala yake, anadai mjibu maombi alimkopesha Rugaibula (mumewe) fedha naye akaweka dhamana hati ya nyumba hiyo. Anadai alipochelewa kulipa, Yusufali alimfungulia kesi.
Hata hivyo, anadai baadaye mume wake alilipa deni hilo wakamalizana na kesi ikaondolewa mahakamani, huku akidai mjibu maombi akikiri hana madai tena kwa aliyekuwa mdaiwa wake.
Alice anadai nyumba hiyo kwa sasa ina thamani ya Sh1.6 bilioni ambayo waliinunua, yeye na mume wake mwaka 2008 kutoka Kampuni ya Quality Real Estate Company Limited.
Katika nyaraka anadai mwaka 2010 Rugaibula alichukua mkopo wa Sh150 milioni kutoka kwa Yusufali akaweka rehani hati ya nyumba kama dhamana ya mkopo huo.
Anadai mume wake alichelewa kulipa mkopo kwa mujibu wa makubaliano, hivyo Yusufali alimfungulia kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yenye namba 208 ya mwaka 2011, akidai aliinunua nyumba, akiwataka waondoke.
Anadai wakati kesi ikisubiri kusikilizwa, Rugaibula alimlipa Sh98 milioni na kutokana na malipo hayo, Yusufali aliiondoa mahakamani kesi hiyo.
Anadai mwaka 2020, Yusufali alifungua shauri la maombi namba 389/2020 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kinondoni dhidi ya Rugaibula na yeye Alice, akidai umiliki wa nyumba hiyo.
Katika utetezi wao wa maandishi anadai walieleza hawakuwahi kusaini makubaliano yoyote ya kuuziana nyumba, bali kulikuwa na makubaliano ya mkopo ambao Yusufali alimkopesha Rugaibula Sh150 milioni.
Baada ya Yusufali kufungua shauri hilo Baraza la Nyumba, anadai mumewe alimlipa kiasi kilichosalia baada ya malipo ya awali ya Sh98 milioni, hivyo kukamilisha malipo yote ya mkopo wa Sh150 milioni.
Anadai pande zote zilifikia makubaliano ya kumalizana, Yusufali akakubali hakuwa na madai tena dhidi ya Rugaibula. Anadai malubaliano hayo yalisajiliwa na baraza kama uamuzi wake na shauri hilo, hivyo likaisha.
Alice anadai baada ya kifo cha mumewe mwaka 2022, aliomba na akateuliwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Temeke kuwa msimamizi wa mirathi Oktoba 16, 2023.
Anadai baadaye alianza kupata malalamiko ya mdomo kutoka kwa wawakilishi wa Yusufali wakieleza nyumba hiyo ni mali yake na yeye ndiye mwenye hati.
Januari, 2025 anadai Yusufali alifungua shauri la maombi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Temeke akiomba nyumba hiyo iondolewe kwenye orodha ya mali za marehemu Rugaibula, lakini baadaye aliliondoa mahakamani shauri hilo.
Anadai mdaiwa wa pili, Msajili wa Hati alitekeleza uhamisho wa nyumba hiyo kutoka jina la Rugaibula kwenda kwa Yusufali licha ya nyaraka za uuzwaji na uhamishaji wake zilikuwa zimeghushiwa.
Anadai akiwa mke wa Rugaibula hakuwahi kutoa ridhaa kuhusu makubaliano ya uuzwaji wa nyumba yanayodaiwa kufanyika na hakuwahi kusaini ridhaa yoyote kuhusu suala hilo.
Anadai tangu waliponunua nyumba hiyo amekuwa akiishi humo mpaka sasa, ingawa mwaka 2012 Yusufali alijaribu kumuondoa katika nyumba hiyo lakini alishindwa.
Anadai mdaiwa wa kwanza, Yusufali amemsababishia usumbufu, msongo wa mawazo na hasara ya kifedha kutokana na kufuatilia mara kwa mara na mateso ya kiakili, hivyo anadai fidia ya jumla.
Mbali ya shauri hilo, Alice amefungua shauri la maombi ya zuio chini ya hati ya dharura, dhidi ya wadaiwa wote akieleza wa kwanza, Yusufali yuko katika hatua ya juu zaidi katika kumuondoa katika nyumba hiyo bila ya uhalali wowote wa kisheria.
Katika shauri hilo namba 24541/2025, anaiomba mahakama itoe amri kumzuia Yusufali, wakala wake, watumishi wake au mtu yeyote atakayemwagiza au kumwelekeza kutomuondoa katika nyumba hiyo, kusubiri maombi hayo kusikilizwa pande zote na pia kusuburi kuamuliwa kwa kesi.
Katika kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Alice anadai Septemba 23, 2025 alivamiwa na kundi la watu na kuwasumbua wapangaji wake wakijaribu kuwafukuza ndani ya nyumba hiyo kwa kuwatupia nje samani na mali zao mbalimbali, bila taarifa yoyote na bila kufuata taratibu.
Anadai licha ya kushindwa katika jaribio hilo la pili baada ya askari polisi kuingilia kati, bado Yusufali anakusudia kumuondoa katika nyumba licha ya kuwapo kesi inayosubiri kusikilizwa.
Anadai kama amri ya zuio isipotolewa, Yusufali ataendelea kutekeleza uamuzi anaoukusudia wa kumuondoa kwenye nyumba hiyo, hivyo masilahi yake katika nyumba hiyo yataathirika kwa kiwango ambacho hakiwezi kufidiwa.