Profesa Nombo ataja mambo matano kuimarisha elimu Afrika

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo ametaja mambo matano ambayo nchi za Afrika zinapaswa kufanya kuinua sekta ya elimu ikiwemo uimarishaji wa mafunzo ya walimu.

Mafunzo hayo ya walimu ni kwenye Tehama na stadi mbalimbali za elimu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na kuandaa wanafunzi watakaokuwa washindani katika soko la ajira.

Profesa Nombo ametaja mambo hayo yakiwa ni sehemu ya makubaliano ya wadau mbalimbali wa elimu Afrika na nje ya bara hilo, wakati akifunga mkutano wa tano wa kimataifa wa Ubora wa Elimu (IQEC) uliofanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 24 hadi 26, 2025 ukiandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet).

Akizungumza kwenye mkutano huo leo Septemba 26, 2025, Nombo amesema kupitia mkutano huo, mataifa ya Afrika yamekubaliana kuongeza rasilimali za ndani ili kufadhili elimu kwa njia endelevu,

Amesema hiyo itasaidia mataifa hayo wakati wa misukosuko ya kiuchumi au mabadiliko ya kipaumbele ya nchi wahisani sekta ya elimu iendelee kubaki imara.

“Pia, tumekubaliana kila nchi kusaidia mageuzi katika mifumo ya ufadhili wa elimu yakiwa yamejikita kwenye vipaumbele vya Umoja wa Afrika (AU) na lengo la nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG).

“Jambo lingine, tumekubaliana kuwa walimu ni kiini cha mageuzi ya ujifunzaji hivyo wanahitaji uwekezaji wa kudumu katika maendeleo yao ya kitaaluma, motisha na ugawaji sahihi wa walimu katika shule mijini na vijijini,” amesema.

Jambo lingine alilotaja Profesa Nombo ni kuongeza uwekezaji kwenye elimu ya awali kama msingi wa ujifunzaji wa maisha yote,

Vilevile, Profesa Nombo amesema sehemu nyingine ya makubaliano hayo ni kuweka vijana, wasichana na makundi yaliyotengwa katika sera za elimu, sio tu kama kama washiriki na wabunifu wa mustakabali wa elimu Afrika

Amesema wizara ya elimu inathibitisha nia ya kuendeleza elimu jumuishi yenye usawa na ubora hapa nchini kwa serikali imetenga asilimia 14 ya bajeti kupitia rasilimali zake za ndani kusaidia uendelevu wa elimu.

“Serikali imepitia mfumo wa sheria ili kuwepo kwa bodi ya walimu  ambayo itaanza kutumika kutoa ushauri kwa wizara na kusimamia maadili ya kitaaluma kw walimu na kuendeleza mafunzo ya mara kwa mara kwa walimu.

Mbali na mambo mengine, Profesa Nombo amesema wadau kwenye mkutano huo wamejadili uchangishaji wa rasilimali za ndani, uhimilivu wa mifumo ya elimu, hamasa ya walimu, usawa katika elimu, teknolojia na sauti za vijana na vijana balehe.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kuimarisha mifumo na uwekezaji: Kusonga mbele katika uhamasishaji wa rasilimali za ndani kwa ajili ya elimu jumuishi, bora na endelevu Afrika”. Profesa Nombo amesema kaulimbiu hiyo imetoa uelewa wa pamoja kuhusu changamoto za rasilimali na fursa zilizopo katika kugema rasilimali hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TenMet, Simon Nanyaro amesema mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha wadau 465 kutoka mataifa 12 ndani na nje ya Afrika.

“Nitoe wito kwa walioshiriki mkutano huu jkwa siku tatu, kile ambacho tumeshirikishana kupitia mkutano huu, kila mmoja ananafasi yake, mtu akitumika,” amesema.