BAO alilofunga mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City limempa mzuka Nassor Saadun wa Azam aliyesema presha ya namba ndani ya kikosi imekuwa kubwa na kufunga kwake kumemuongezea morali.
Saadun aliifungia timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 jingine likifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Saadun alisema presha ya namba imekuwa kubwa kutokana na ongezeko la wachezaji hasa eneo la ushambuliaji lililo na Japhte Kitambala.
“Msimu mpya kocha mpya na kuna maingizo mengi mapya. Siyo rahisi kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu kocha hajauliza historia anapambana kujenga kikosi chake,” alisema Saadun ambaye msimu uliopita alifunga mabao manane na kuasisti mara tatu katika ligi.
“Kila nafasi nitakayoipata nitahakikisha naifanyia kazi kwa kufuata maelekezo (ya kocha) lengo ni kuwa na mwendelezo wa ubora kama msimu uliopita,” aliongeza Saadun aliyewika na Geita Gold.
Saadun alisema hana hofu ya kutua kwa wachezaji wapya kwani wanampa nguvu ya kupambana zaidi na kwamba anatamani kupata nafasi zaidi ya kuonyesha vitu vyake uwanjani kama alivyoaminiwa dhidi ya Mbeya City na kufanikiwa kufunga mojawapo kati ya mabao mawili.
“Ligi ndio kwanza imeanza, lakini pia tuna mashindano ya kimataifa. Ni muda sahihi kwake kupambana kwenye uwanja wa mazoezi na mechi za mashindano ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata namba chini ya kocha Florent Ibenge,” alisema.