SIMBA ilikuwa uwanjani usiku wa jana kuvaana na Fountain Gate katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, lakini kabla ya hapo kambini kuna maisha mapya yameanza chini ya Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ na inaelezwa, jamaa amewasapraizi mastaa wa timu hiyo.
Wanafainali hao wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, imeanza maisha mapya kabla ya Kocha Fadlu Davids na baadhi ya wasaidizi aliokuwa nao waliotimkia Raja Casablanca ya Morocco, klabu aliyokuwa akiinoa kama kocha msaidizi kabla ya kutua Msimbazi Julai mwaka jana.
Kuondoka ghafla kwa Fadlu kumeulazimisha uongozi wa Simba kumpa kazi Morocco ambaye ni kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars akisaidiana na Seleman Matola ambaye jana aliiongoza katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.
Sasa inaelezwa mara baada ya mabosi wa Simba kumtangaza Morocco kama kaimu kocha mkuu hadi atakapopatikana kocha mkuu, jamaa alitimba kambini na kuanza mambo na kuna mambo yamekuwa ni sapraizi kwa wachezaji kwa mabadiliko aliyowafanyia kabla ya jana kushuka uwanjani.
Sapraizi aliyowafanyia wachezaji, huenda pia ikaonekana katika pambano la marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana ambao ndio mwanzo wa kibarua cha kocha huyo kuziba nafasi ya Fadlu aliyeanza kazi katika klabu ya Raja Casablanca.
Morocco ameachiwa mechi hiyo ya CAF na Simba inahitaji kulinda ushindi wa bao 1-0 iliyopata ugenini wikiendi iliyopita kutokana na Matola kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa ugenini, hivyo kutoruhusiswa kukaa katika benchi.
Kwa kutambua kibarua hicho kinachosubiriwa kwa hamu na wanasimba kutaka kuona kama ataweza kuivusha timu kwenda raundi ya pili, kocha Morocco inadaiwa alitimba kambini Mo Bunju Arena na kufanya mabadiliko fulani ambayo mastaa wa timu hiyo wameyaanika kwa Mwanaspoti.
Inaelezwa moja ya sapraizi ni kocha kuzungumza na wachezaji kirafiki na kuwaambia hakuna maajabu makubwa anayoweza kufanya zaidi ya wao kujitoa kwa asimilia zote Jumapili mbele ya wapinzani wao ili kwenda raundi ya pili na mambo yawe mepesi.
Pia amewasisitizia heshima ya Simba ipo mikononi mwao na lazima wajitoe kuwapa raha mashabiki wa Simba na kuwadhibitishia kuwa, kuondoka kwa Fadlu sio ishu kubwa kwao, kwa vile Simba itaendelea kuwepo na imewaajiri kuhakikisha inatimiza malengo kwa msimu mpya wa 2025-2026.
Mmoja kati ya mastaa wa kigeni wa klabu hiyo, aliliambia Mwanaspoti kwamba hali ya ndani ya kikosi hicho ni shwari, kutokana na Morocco kuwatuliza presha kwa kuanzia kubadilisha saikolojia yao kujiandaa na vita iliyopo mbele yao, kwani awali kuondoka kwa Fadlu kuliwachanganya.
Kiungo huyo, alisema kuwa kocha huyo ambaye ni kocha wa Taifa Stars, amewaambia anataka kuona wanajiamini na wala hakuja hapo kubadilisha mambo mengi kwa kuwa anashika majukumu hayo kwa muda tu.
“Morocco anataka kila mchezaji kujituma na kufurahia nafasi ya kuichezea Simba kwa kila mmoja kuonyesha uwezo wake ili kuisaidia Simba,” alisema nyota huyo wa kigeni na kuongeza;.
“Ni mtu mzuri kila mmoja amemfurahia, ametuonyesha heshima kubwa, ametutataka kuondoa wasiwasi maisha ya soka ndivyo yalivyo. Leo imetokea kwa makocha kuondoka, lakini hata sisi kama wachezaji tunaweza kupita njia hiyo hiyo.
“Kitu kikubwa ametaka kuona tunabadilika kwa kurudisha akili zetu uwanjani, amesema kila mmoja wetu ana kiwango kikubwa, ndio maana tumesajiliwa Simba, anataka kuona tunaonyesha uwezo wetu wote kwa ajili ya timu.” alisisitiza nyota huyo.
Mchezaji mwingine ambao yupo na kikosi hicho tangu msimu uliopita, alisema namna kocha alivyozungumza na alivyokuwa akiwanoa sambamba na Matola anahisi kuna kitu tofauti kinaweza kutokea katika mechi ijayo ya kimataifa, ili Simba kufanya makubwa japo ni muda mfupi kwao.
“Hata wachezaji tumehisi unafuu flani na tunaenda katika mechi ya Ligi kwa kiu ya kufanya makubwa kabla ya kuigeukia pambano la marudiano la CAF ambalo, hata sisi tunahisi hatukucheza vile ilivyotarajiwa. Hii ilitokana na uchovu, kwani hatujapata muda mzuri wa kujiandaa,” alisema mchezaji huyo na kuongeza;
“Kwa mashabiki wa Simba wakae tu wakijua Simba ina sapraizi yao Jumapili, kama ambavyo sisi kocha Morocco na wenzake walivyotusapraizi mazoezini. Sio kila kitu lazima tuseme, ila jiandae kushuhudia mpira mwingi.”
Mwanaspoti lilimtafuta Morocco, ambaye alikiri kuanza na kazi ya kurekebisha saikolojia ya wachezaji akisema mwanzo huo umetokana na kugundua wachezaji wengi walikuwa na mawazo baada ya kocha aliyekuwepo na wenzake kuondoka bila kutarajiwa.
“Nilikuwa na makocha wenzangu niliowakuta Seleman Matola na yule wa mazoezi ya utimamu wa mwili, tuliona namna saikolojia ya wachezaji ilikuwa chini kwanza, kwa hiyo tukaona tuanzie hapo,” alisema Morocco nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na Coastal Union.
“Mimi sio malaika, ni kocha tum, nimewaambia nataka kuona kila mchezaji anajituma kwa ajili ya Simba, kila mmoja ana nafasi ya kuitumikia hii klabu kubwa,” alisema Morocco na kuongeza; “Nitaendelea kuwa na vikao vya kuwajenga wachezaji mmoja mmoja kila baada ya vipindi vya mazoezi ili kuwaongezea uwajibikaji, ili kuona katika kipindi hiki cha kufanya kazi pamoja tunaleta mafanikio na furaha kwa Wanasimba kwa ujumla.”
Mara baada ya mechi ya jana usiku, Simba itajiandaa kwa mechi ya Jumapili dhidi ya Gaborone, kisha kurudi tena katika pambano la pili la Ligi Kuu Jumatano ijayo ikiikaribisha Namungo kabla ya ligi kusimama ili kupisha mechi za kirafiki za kimataifa.