Arusha. Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Arusha, Frank Mlinzikutwe amewataka wananchi kuhakikisha wanamiliki hati miliki za ardhi ili kupata uhalali wa kisheria na kuondoa migogoro ya umiliki.
Kamishna huyo ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 26, 2025 alipokuwa akikabidhi hati miliki za ardhi kwa askari wa Jeshi la Polisi kupitia kupitia Chama cha Ushirika wa akiba na mikopo cha usalama wa Raia (Ura Saccos).
Amesema hati miliki hutoa fursa mbalimbali ikiwemo za mikopo katika taasisi za kifedha pamoja na kuondoa migogoro ya mara kwa mara inayotokana na kutokuwa na nyaraka halali za umiliki wa ardhi.
Amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kununua maeneo ambayo yamepangwa na kupimwa ili waweze kupatiwa hatimiliki zinazowasaidia katika mambo mengi ikiwemo kuepusha migogoro ya ardhi ambayo imekithiri maeneo mengi nchini.
“Tunahamasisha wananchi kuwa na miliki za maeneo yao ili kunapokuwa na mgogoro badala ya kusema hili eneo ni langu unakuwa na nyaraka inayokuthibitishia eneo lako,inakusaidia kupata mkopo kufanya uendelezaji na masuala mengine.
“Hatutaki askari aache kazi ya kufanya ulinzi wa nchi ageuke kufuatilia hati kila siku na hili litasaidia wanachama badala ya kutumia muda mwingi kwenda kutapeliwa mtaani watakuwa na uhakika wa kupata viwanja vilivyopimwa na kupangwa,” amesema.
Kamishna huyo amesema kwa sasa Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi imeanza mchakato wa kutoa hati kwa njia ya kielktroniki ambapo mtu anaweza kuomba hati kwa njia ya mtandao na akikamilisha nyaraka zote anapata hati siku hiyo hiyo.
Meneja wa Ura Saccos mkoa wa Arusha, Koplo Chiunda David amesema Saccos hiyo yenye wanachama zaidi ya 47,000 kote nchini na kuwa Aprili mwaka huu imeingia makubaliano na taasisi ya Tanzanite Crater City kwa lengo la kuwawezesha wanachama wake kununua viwanja kwa punguzo la bei.
Amesema kupitia makubaliano hayo wanachama wanawauziwa viwanja ambavyo vimepimwa na kuwa hadi sasa wanachama zaidi ya 30 wameshanunua viwanja hivyo.
“Baada ya kuingia makubaliano na mpaka sasa wanachama zaidi ya 30 wameshanunua viwanja hivyo na tunayo furaha kukabidhiwa hati katika awamu hii ya kwanza,” amesema.
“Lengo la ushirika huu ndani ya Jeshi la Polisi tangu ulipoasisiwa mwaka 2006 ni kumkomboa askari na familia yake kiuchumi ikiwemo kumuwezesha mwanachama kumiliki makazi yaliyopimwa na kupatiwa hati,”
Amesema Serikali imekuwa ikisisitiza wananchi kumiliki viwanja vilivyopimwa na kupatiwa hati na kuwa wao waliona ni fursa kuungana ili wanachama wake wapate viwanja kwa bei nafuu.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Arusha na wanachama wenzake, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Alphonce Bandya, alishukuru kwa makubaliano baina ya Saccos yao na taasisi hiyo kwani imewawezesha kumiliki ardhi.
“Ninayo furaha kukabidhiwa hati hizi kwa niaba ya wanachama wenzangu kwani zamani ilikuwa shida baadhi ya askari kumiliki vitu kama hivi,tunayo furaha kwani tunajikwamua na kupata makazi,”amesema.
“Tunapongeza chama chetu kimetusaidia kupata fursa hii na tumesikia kuna mradi mwingine, tunasubiri tukipewa maelezo zaidi tutahamasishana ili tunufaike na kuondokana na adha ya kukosa makazi,”ameongeza.
Awali Mkurugenzi wa Tanzanite crater city, Deogratias Michael, amesema mradi huo upo Kata ya Oljoro, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na kuwa lina ukubwa wa zaidi ya ekari 1,000 ambapo kuna viwanja kwa ajili ya makazi, makazi na biashara, biashara na huduma za kijamii kama shule.
Amesema bei za viwanja hivyo ni nafuu kwa mahitaji ya jamii na ziliwekwa kwa makubaliano kupitia halmashauri.
“Tunashukuru Ura Saccos kwa kuchangamkia fursa hii kwa wanachama wake na tutawafikia wanachama wake Tanzania nzima ila kwa kuanzia tumeanza na Arusha ,”amesema.