Tabia ndogo za afya zinazoweza kuokoa maisha yako

Dar es Salaam. Kila mwaka duniani kote, mamilioni ya watu hufariki kutokana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa takribani watu milioni 41 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa haya, sawa na asilimia 74 ya vifo vyote duniani.

Habari njema ni kwamba magonjwa haya mengi yanaweza kuzuilika ikiwa mtu atajihimu kuzingatia kupitia tabia ndogo ndogo kwa kila siku.

Kula mlo bora usio na mafuta mengi

Lishe duni ni chanzo kikuu cha magonjwa yasiyoambukiza. Ripoti ya WHO ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa watu zaidi ya bilioni moja duniani wana uzito kupita kiasi, hali inayoongeza hatari ya kupata kisukari cha aina ya pili na shinikizo la damu.

Tabia rahisi na ndogo unazoweza kuzifanya eneo hili ni pamoja na kula  mboga na matunda angalau mara tano kwa siku na kupunguza kama sio kuacha vyakula vya kukaanga, vyenye sukari nyingi na vyakula vya haraka.

Mtaalamu wa magonjywa yasiyoambukiza, Dk Omary Ubuguyu anasema udhibiti wa kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza, unahitaji mfumo maalumu wa maisha ikiwamo kufahamishwa dalili za magonjwa hayo na umuhimu wa kupima na kuzingatia mfumo bora wa maisha kama vile lishe na kufanya mazoezi.

Kusoma taarifa za onyo kwenye vifungashio vya vyakula

Ni wananchi wangapi wenye tabia ya kusoma maelezo ya viambata vya bidhaa za chakula yaliyomo sehemu ya mbele ya vifungashio na kujua maana yake na kuchukua hatua?

Wanaojitahidi utakuta wale wanaotazama tarehe ya mwisho wa matumizi ya bidhaa husika na si taarifa nyingine. Ni muhimu kwa walaji na wananchi kwa jumla kujenga mazoea ya kutambua kilichomo ndani ya bidhaa wanayonunua.

Hata hivyo, taarifa hii ya lishe inayoonyesha viambata vilivyomo kwenye chakula inapaswa kuwa fupi na iwekwe kwa namna rahisi kueleweka, mara nyingi kwa kutumia alama za rangi, alama za nyota, au nembo maalum.

Magonjwa yasiyoambukiza yanachochewa zaidi na ulaji usiofaa wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, sukari kupita kiasi na nishati nyingi. 

Taarifa hizi zina uhusiano wa karibu na magonjwa haya kwa kuwa huonya mlaji endapo chakula kimejaa sukari, chumvi au mafuta, ambavyo ni vihatarishi vikuu vya magonjwa haya.

Ni taarifa zinazomsaidia mnunuzi. Kwa mfano, mtu akiwa dukani anaweza kuchagua soda yenye sukari kidogo au siagi yenye mafuta kidogo kwa kuangalia alama za mbele ya pakiti.

Kubwa zaidi kadri watu wanavyozidi kuelewa alama hizi, ndivyo jamii inavyopunguza ununuzi wa vyakula visivyo na afya na hivyo kupunguza mzigo wa magonjwa ya kuambukiza.

“Magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto kubwa ya karne hii… Alama za tahadhari mbele ya kifurushi ni njia madhubuti za afya ya umma zinazopaswa kutumika,’’ anasema mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu afya, Dainius Pūras.

Maji ni uhai, na kunywa maji ya kutosha husaidia mwili kufanya kazi kwa ufanisi. Kwa mujibu wa chapisho la  National Academies of Sciences, Engineering, and Medicine  la mwaka 2020, wanaume wanashauriwa kunywa takribani lita 3.7 kwa siku na wanawake lita 2.7.

Kukosa maji ya kutosha kunaweza kuathiri afya ya figo na kuongeza uwezekano wa kupata mawe kwenye figo, ambayo ni tatizo linaloongezeka kila mwaka. Kumbuka, badala ya soda na juisi zilizojaa sukari, chagua maji safi au juisi za matunda zisizoongezwa sukari.

Fanya mazoezi mara kwa mara

Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa afya, kufanya mazoezi kwa dakika 30 kila siku kunaweza kupunguza hatari ya kupata kisukari kwa zaidi ya asilimia 40.

Mazoezi hayamaanishi lazima kwenda maeneo maalum kwa ajili hiyo. Kutembea, kupanda ngazi badala ya kutumia lifti, kulima bustani au kucheza michezo ya kujifurahisha ni mbinu rahisi za kuongeza mwendo wa mwili. Na haya unaweza kufanya katika mazingira yoyote iwe mjini au kijijini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza angalau dakika 150 za mazoezi ya kiwango cha wastani kwa wiki. Hii ni sawa na dakika 30 tu kila siku tano kwa wiki jambo ambalo mtu yeyote anaweza kulifanya.

Kudhibiti msongo wa mawazo

Msongo wa mawazo sugu unaweza kuongeza shinikizo la damu na kusababisha matatizo ya moyo. Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Lancet mwaka 2016 ulionyesha uhusiano mkubwa kati ya viwango vya juu vya msongo wa mawazo na ongezeko la magonjwa ya moyo.

Njia rahisi za kudhibiti msongo ni pamoja na kupumua kwa kina na kufanya mazoezi ya kutuliza mwili kama yoga au tahajudi, kupanga muda wa kupumzika na kujifurahisha na familia au marafiki na kuweka ratiba nzuri ya kazi na kulala kwa kiwango cha kutosha.

Kulala kwa kiwango cha kutosha

Watu wengi huchukulia usingizi kama jambo rahisi, ilhali ni nguzo kuu ya afya. Inaelezwa kuwa kulala chini ya saa sita  kwa usiku huongeza hatari ya kupata kisukari na unene kupita kiasi. Watu wazima wanashauriwa kulala kati ya saa 7–9 kila usiku.

Kila siku tunayo nafasi ya kuchagua tabia ambazo ama zinaimarisha au kudhoofisha afya zetu. Kula vizuri, kunywa maji ya kutosha, kufanya mazoezi, kuepuka sigara na pombe, kudhibiti msongo, kulala vya kutosha, kupima afya mara kwa mara na kudumisha usafi na mangine ambayo hayakutajwa hapa; vyote hivi ni tabia rahisi na ndogo lakini vyenye nguvu kubwa ya kuokoa maisha.

Kama anavyosema Mkurugenzi Mkuu wa WHO,  Dk Tedros Ghebreyesus, “Afya bora inaanza na hatua ndogo tunazochukua kila siku.”