Tumaini jipya elimu kuoanishwa Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Wahitimu wa Kitanzania, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya ajira, sasa wanaweza kuzitafuta Kenya,Uganda au kwingineko Afrika Mashariki kutokana na kuwekwa mfumo wa pamoja wa mikopo na vigezo vya pamoja vya masomo.

Vivyo hivyo, mwanafunzi aliye katikati ya muhula wa masomo Tanzania anaweza kuhamia chuo kikuu nchini Rwanda au Burundi na kuendelea na mwaka huohuo bila kushuka daraja.

Hii ni kutokana na mpango chini ya Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), ambao umeweka viwango na vigezo vya pamoja, ili kurahisisha uhamaji wa kitaaluma na kikazi katika kanda.

Huu ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na janga la pamoja na ukosefu wa ajira.

Wiki iliyopita, mawaziri wa elimu, watunga sera na viongozi wa vyuo vikuu walikutana Munyonyo, Uganda, katika mkutano wa kwanza wa mawaziri wa kikanda kuhusu elimu ya juu.

Dhamira yao ilikuwa “kuoanisha mifumo ya elimu ya juu kitaifa, kuoanisha sifa za kitaaluma na kuunda eneo la pamoja la elimu ya juu Afrika Mashariki.”

“Hii ndiyo maana ya uoanishaji,” amesema Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa, alipozungumza na gazeti dada la The Citizen leo Septemba 25, 2025.

“Inaruhusu uhamaji wa wanafunzi na wahadhiri na kuhakikisha sifa zetu zinatambulika kila mahali katika ukanda,” amesema.

Kwa maneno rahisi, mhitimu anayepata shahada Dar es Salaam sasa anaweza kuomba kazi Nairobi, Kampala, Kigali au Bujumbura bila wasiwasi wa elimu yake kutopewa thamani au kushushwa daraja.

Kwa wahitimu wanaopambana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, hii ni fursa mpya. Shirika la Kazi Duniani (ILO) liliripoti mwaka 2023 kwamba zaidi ya vijana milioni 72 barani Afrika hawakuwa kazini, shule, wala kuwa na mafunzo.

Katika Afrika Mashariki, ukosefu wa ajira miongoni mwa wahitimu umeendelea kuwa tatizo, kwa kiasi kikubwa ikiwa ni kutokana na kutooana kwa mifumo ya elimu na soko la ajira. Mfumo huo wa pamoja unaweza kuondoa vizuizi hivyo.

Mtafiti wa masuala ya elimu mkazi wa Arusha, Dk Joseph Mbawala ameeleza hatua hiyo kama “fursa ya kihistoria.”

“Kwa miaka mingi, ukosefu wa utambuzi wa shahada katika ukanda uliwalazimisha vijana kutafuta uhalali nje ya Afrika. Sasa, kwa hatua hii, ukanda wenyewe unakuwa soko,” amesema.

Ukosefu wa ajira miongoni mwa wahitimu wa Kitanzania umekuwa changamoto ya muda mrefu. Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha takribani vijana 800,000 huingia sokoni kila mwaka, lakini ni sehemu ndogo tu hupata ajira rasmi.

Uoanishaji elimu unaweza kufungua njia. Wataalamu wanasema sekta ya teknolojia ya Kenya, sekta ya mafuta na gesi inayoendelea kukua Uganda na mkakati wa mabadiliko ya kidijitali Rwanda, vyote vinahitaji nguvu kazi ya kikanda.

Kwa Watanzania, uwezo wa kushindana katika soko la ajira kwa sifa zinazotambulika kote, kunaweza kuwa mabadiliko ya kimsingi.

Hata hivyo, wataalamu wanatahadharisha kuwa, uhamaji pekee hautoshi.

“Wahitimu wetu lazima wawe tayari kukidhi viwango vya soko la kikanda,” amesema mshauri wa elimu, Dk Asha Nduguru na kuongeza:

“Hii inamaanisha mafunzo bora katika stadi tete (soft skills), maarifa ya kidijitali na lugha kama Kifaransa, ambayo ni muhimu katika nchi jirani kama Burundi na Rwanda nayo ni muhimu.”

Zaidi ya kuwasaidia wahitimu mmoja mmoja, uoanishaji unaweza kuliinufaisha Taifa. Vyuo vikuu vya Kitanzania vinaweza kuvutia wanafunzi zaidi kutoka ukanda mzima, jambo linaloongeza mapato na kukuza ubadilishanaji wa elimu.

Tayari, maprofesa na wahadhiri wa Kitanzania wanaweza kufundisha katika nchi nyingine za EAC bila kushushwa madaraja.

“Ushirikiano wa wafanyakazi na utaalamu ni muhimu,” Profesa Kihampa amesema na kuongeza:

“Mwalimu kutoka Tanzania anatambulika kama profesa kila sehemu ya ukanda. Hii si tu kuwawezesha wasomi wetu, bali pia kuinua ubora wa elimu ya juu kwa ujumla.”

Dira ya EAC 2050 inaweka bayana kuwa uunganishaji wa elimu ni msingi wa ustawi wa kikanda. Kupitia uoanishaji wa mitalaa, sifa na mikopo, jumuiya inalenga kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi na inayoweza kuhama, tayari kukabiliana na mahitaji ya karne ya 21.

Pamoja na hatua hii, changamoto bado zipo. Nchi zinatofautiana katika uimara wa mifumo yake ya elimu ya juu. Kenya, kwa mfano, ina sekta kubwa zaidi ya vyuo vikuu binafsi.

Hivyo, Tanzania italazimika kuhakikisha vyuo vyake vinabaki na ushindani katika soko la kikanda lililofunguka.

Vilevile, kuna suala la kitamaduni. Kihistoria, Watanzania wamekuwa waangalifu kuhusu uhamaji. Wahitimu wachache hufikiria kuhamia nje lakini zaidi ya Afrika, mtazamo unaoweza kupunguza fursa.

“Tukiendelea kujizuia, nchi nyingine zitachukua sehemu kubwa ya manufaa,” amasema Dk Mbawala na kuongeza:

“Tunapaswa kuwahamasisha wahitimu wetu kuukumbatia uhamaji wa kikanda kama sehemu ya mkondo wa taaluma zao.”

Vilevile, Serikali zinapaswa kushughulikia hatari ya upungufu wa wataalamu ikiwa idadi kubwa ya wataalamu wa Kitanzania wataondoka kwa ajili ya mishahara mikubwa kwingineko, uchumi wa ndani unaweza kudumaa.