Uandishi wa habari matumizi ya nishati jua kwenye kilimo waongezeka Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini nchi tatu za Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda, zimekuwa na ongezeko la uandishi wa habari za matumizi ya umeme jua katika kilimo.

Utafiti huo ni kulingana na ripoti iliyotolewa na Kituo cha Umahiri kwenye vyombo vya habari (African Centre for Media Excellence) ukifadhiliwa na Taasisi ya MOTT (MOTT Foundation) ikionyesha, Tanzania kushika nafasi ya tatu ya uandishi wa habari hizo, nyingi zikitokana na matukio na hakuna habari zozote za uchunguzi.

Kenya imeongoza miongoni mwa nchi hizo kutoa habari 43 za matumizi ya umeme wa jua kwenye kilimo ikiwa ni asilimia 38.1, Uganda  habari 36 sawa na asilimia 31.9 huku Tanzania ikishika nafasi ya tatu ikiwa imechapisha habari 34 sawa na  asilimia 30.1.

Akizungumza leo Septemba 26, 2025  katika uzinduzi wa ripoti hiyo Dar es Salaam, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, Dk Darius Mukiza amesema utafiti huo umefanyika kuanzia Januari Mosi hadi Desemba 2024.

Utafiti ulihusisha gazeti la Mwananchi linalochapishwa na  Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa upande wa Tanzania.

Kwa nchi ya Kenya, vyombo vya habari vilivyotumika ni gazeti la Daily Nation, Shirika la Taifa la Utangazaji (KBC) na upande wa Uganda, ni Shirika la Taifa la  Utangazaji (UBC) na gazeti la Newvison.

“Habari za matumizi ya umeme wa jua kwenye kilimo zimeongezeka kwa asilimia 79 kutoka habari 63 mwaka 2023  hadi 113 mwaka 2024, pamoja na ongezeko hilo uandishi umeegemea zaidi habari za matukio yaliyohusisha Serikali, mashirika binafsi.

“Habari za uchunguzi na zilizofanyiwa tathmini ya kina hazikuonekana kwenye vyombo hivyo wakati utafiti ukifanyika,” amesema Dk Mukiza akiwasilisha ripoti hiyo.

Gazeti la Mwananchi pekee ambalo limetumika kwenye utafiti huo, liliachapisha habari hizo kwa asilimia 52.9 ikifuafiwa na TBC  kwa asilimia 47.1.

Dk Mukiza amesema jambo lingine walilobaini wakati wa utafiti huo, habari za matumizi ya nishati jua kwenye kilimo hazikuonekana kama habari za kuvutia wateja hivyo, hazikupata nafasi za mwanzo ndani ya vyombo vya habari.

“Pia, habari zilizochapishwa hazikuzingatia usawa wa kijinsia, asilimia 72.2 ya habari zilimnukuu zaidi ya mtu mmoja mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo ni asilimia 32 pekee, sauti za wanaume zilikuwa asilimia 74, Kenya wanawake wamehusishwa mara nyingi kwenye habari ikilinganishwa na Uganda na Tanzania,” amesema.

Akizindua utafiti huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEC), Deodatus Balile amesema habari za matumizi ya umeme wa jua kwenye kilimo zinahusisha kwenye umwagiliaji, ukaushaji wa mazao kwa lengo la kusafirisha nje ya nchi.

Amesema licha ya kuonekana kwa ongezeko hilo habari za uchunguzi bado ni changamoto upatikanaji wake.

Matumzi ya sola kwenye kilimo zipo faida apatazo mtumiaji kulingana na wataalamu mbalimbali  ikiwamo kukausha viungo kwa asilimia 70 kwa kila kirutubisho kwenye mazao, kwa sababu hairuhusu kupenya kwa mionzi ya jua.

Pia, sola hairuhusu mionzi ya jua ukianika karafuu na mdarasini, ukianika juani inaondoa uhalisia hata kibiashara inakuwa ngumu.