Unatunzaje kitovu cha mtoto anapozaliwa?

Kitovu cha mtoto mchanga baada ya kuzaliwa ni sehemu nyeti inayohitaji uangalizi wa karibu, ili kuhakikisha mtoto anakua salama bila kupata maambukizi. 

Baada ya kuzaliwa na kutenganishwa na kondo la nyuma la mama, kitovu hubaki kikiwa kimefungwa kwa kitambaa maalum au kipande cha plastiki na huchukua siku kadhaa kabla ya kukauka na kuanguka.

Mkuu wa kitengo cha mama na mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama,  Dk Laizer Philip anasema hatua hii, ingawa ni ya kawaida kwa kila mtoto, bado hubeba hatari endapo hakutakuwa na uangalizi wa kutosha kutoka kwa wazazi au walezi.

Utunzaji sahihi wa kitovu

Anasema kitovu kinapaswa kuachwa kikauke chenyewe bila kufungwa kwa vitambaa au kufunikwa na vitu visivyo safi.

Anasema baada ya mtoto kutenganishwa na mama, kitovu kinaweza kukatika ndani ya siku tano, wiki moja hadi wiki mbili kulingana na changamoto mbalimbali.

 “Mtoto anapozaliwa kuna kitu tunaita kondo la nyuma, ambacho ni kiunganishi kati ya mama na mtoto, kupitia kwenye kitovu cha mtoto, kwa hiyo mishipa ya damu inayotoka kwa mama inayosafirisha chakula kwenda kwa mtoto hutumia njia ya kitovu. Kondo hili hutengenezwa katika wiki ya 20 mtoto anapokuwa tumboni,”anasema.

Anataja sababu za kuchelewa kukatika kwa kitovu cha mtoto kuwa kunaweza kusababishwa na maambukizi ya bakteria,  wanaosababishwa na usafi duni wakati wa utunzaji wa kitovu cha mtoto.

Kwa mujibu wa Dk Philip, zipo changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kukatika kitovu cha mtoto ikiwa ni pamoja na sehemu ya pembeni ya kitovu kutoa usaha, mwonekano wa wekundu unaozunguka kitovu au majimaji yenye harufu kali.

Anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia dawa za kienyeji wanapoona dalili za hatari kwenye kitovu cha mtoto,  ikiwa ni pamoja na kupaka kinyesi cha ng’ombe hali ambayo ni hatari kwa afya ya mtoto.

“Mama baada ya kujifungua huwa tunampa elimu ya namna ya kuishi na mtoto kwa usalama na kuzingatia usafi na tunawashauri wanapoona dalili sio nzuri wawarudishe hospitali, ” anaeleza na kuongeza: 

“Wakati mwingine kitovu kinaweza kukatika lakini kukabaki na kinyama chekundu au cha pink (rangi ya waridi), kitu hiki kinaweza kuisha baada ya muda au kikaendelea kuwepo, huyu mtoto tunasema arudishwe hospitali mara moja.” 

Dalili za hatari katika siku saba za kwanza

Dk Philip anasema dalili zinazoweza kuashiria tatizo kwenye kitovu cha mtoto mchanga, ni pamoja na utokaji wa damu usiokoma kwenye eneo la kitovu, kuvimba kwa kitovu au ngozi kuzunguka eneo hilo na kuwa nyekundu.

Sababu nyingine ni kutoa usaha au harufu mbaya, mtoto kupata homa au kuonekana mchovu kupita kawaida pamoja na kulia mara kwa mara kila anapoguswa eneo la kitovu. 

Anashauri kuwa mara mama anapobaini moja ya dalili hizo, amwahishe mtoto kwenye kituo cha kutolea huduma za afya.

Kumsafisha mtoto mchanga 

Dk Philip anaeleza kuwa mtoto anapozaliwa hapaswi kuogeshwa, kwani anazaliwa na mafuta yake ya asili yanayomsaidia kutunza joto la mwili.

Anasema: “Mtoto anapozaliwa huwa haogeshwi, kwa sababu anazaliwa na hali ya ubichi ubichi, na mafuta yanayotunza joto kwenye mwili wake. Sasa badala ya kumuogesha tunatumia mafuta maalumu kumsafisha ili aendelee kupata joto taratibu wakati anapozoea mazingira mapya ya duniani, mpaka kitovu kinapoanguka ndipo anaogeshwa.”

Kuna dhana ya ukosefu wa nguvu za kiume pale kitovu cha mtoto mchanga wa kiume, kinapokatika na kuangukia kwenye sehemu yake ya uume.

Dk Philip anasema: “Kwenye vitabu vyote nilivyosoma sijawahi kukutana na hicho kitu, wala uthibitisho wowote wa kisayansi kwamba kitovu cha mtoto wa kiume kikikatika na kuangukia kwenye uume wake anaishiwa nguvu za kiume.”

Anasema hizo zinaweza kuwa ni imani kwa baadhi ya makabila, zinazolenga kumpa mama umakini wa kujua ni lini na wapi kitovu cha mtoto kilikatika na kutunza usafi wa mtoto na mazingira yake.