Dar es Salaam. Wataalamu wa elimu nchini wamesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na kufikiria upya dhana ya maarifa ya kusoma na kuandika, ili kuendana na mahitaji halisi ya ulimwengu wa kidijitali.
Wanasema iwapo taifa linataka kuwaandaa vijana kwa ufanisi kukabiliana na changamoto na fursa za karne ya sasa, basi maarifa hayo lazima yaende sambamba na ujuzi wa kisasa unaohitajika katika zama hizi za teknolojia.
Kauli hiyo imetolewa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kusoma na Kuandika ambayo yamefanyika wiki hii jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Elimu (AKU-IED), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani na Chama cha Walimu wa Lugha ya Kiingereza Tanzania (TETLA).

Akizungumzia kuhusu maarifa ya kusoma na kuandika, mhadhiri wa walimu na mtaalamu wa masuala ya kusoma na kuandika kutoka AKU-IED, Dk Samuel Andema, amesema tafsiri hiyo sasa imekuwa finyu katika dunia inayoongozwa na teknolojia za kisasa na utofauti wa tamaduni.
“Kihistoria, kusoma na kuandika kulimaanisha uwezo wa kusoma na kuandika maandiko, lakini wasomi wamegundua kuwa uelewa ni mpana zaidi.
“Siyo ujuzi wa kiufundi pekee, bali pia ni utamaduni na desturi ya kijamii inayodhihirisha mamlaka, utambulisho na ushiriki.”
Alibainisha kuwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, wasomi wa “maarifa mapya” wamekuwa wakisema teknolojia inabadilisha namna uelewa huo unavyofanya kazi.
“Watu wa leo hawatakiwi tu kusoma na kuandika, bali pia kutafsiri picha, video, alama za kitamaduni na hata miingiliano ya kidijitali.

“Mtu anaweza kuwa mahiri kusoma na kuandika, lakini akipelekwa mbele ya baraza la wazee kuhusu masuala ya kitamaduni, anaweza kuonekana mjinga kwa sababu hawezi kushiriki kwenye muktadha huo,” ameeleza na kuongeza;
“Kusoma na kuandika ni msingi, lakini vinapaswa kufundishwa sambamba na ujuzi wa kidijitali, maarifa ya kitamaduni na fikra makini,” amesema Dk Andema.
Kwa upande wake Mkuu wa AKU-IED, Dk Jane Rarieya, alieleza kwa uwazi:
“Kwa upande mmoja, teknolojia za kidijitali zinatoa fursa kubwa za kupata elimu hata maeneo ya mbali na kuwapa nguvu wanafunzi. Lakini, si kila mtu anaweza kumudu au kufikia teknolojia hizi,” alisema.

Amesema kuwa maarifa ya kidijitali lazima yaende sambamba na uwajibikaji.
“Teknolojia inaweza kutumika vibaya. Tumeona akili bandia ikiwasukuma vijana kwenye maamuzi hatarishi, hata ya kujiua. Kuwa na maarifa ya kidijitali maana yake ni kuwa salama, mkosoaji na mwenye kuwajibika mtandaoni,” amesema.
Amesema licha ya Serikali kupiga hatua katika kuongeza uandikishaji na upatikanaji wa elimu, bado kuna wanafunzi wengi wanamaliza shule ya msingi bila kuelewa vizuri kusoma.
“Na katika mijadala ya kitaifa, mara nyingi maarifa ya kusoma na kuandika huangaliwa tu kwa msingi wa “maneno matatu”: kusoma, kuandika na kuhesabu,” amesema.
Mchambuzi wa elimu, Dk Asha Mkwizu, amesema mtazamo wa maarifa ya kusoma na kuandika unaweza kulikwamisha taifa.
“Iwapo tutaendelea kuchukulia kusoma na kuandika kama ujuzi wa kusoma na kuandika pekee, tutalea kizazi kilicho na uelewa wa kimsingi, lakini kisicho na uwezo wa kidijitali,” amesema.