Vijiji 7,604 vyasalia kumilikishwa hati za hakimiliki za kimila

Shinyanga. Vijiji 7,604 nchini vimesalia ili kukamilisha idadi ya vijiji vyote 12,333 nchini katika mpango wa matumizi ya ardhi uliolenga kuongeza thamani ya ardhi, kuwakwamua wananchi katika wimbi la umasikini pamoja na kuweka suluhu ya kudumu ya migogoro ya ardhi iliyoota mizizi katika maeneo mbalimbali.

Mpaka sasa kitaifa kuna jumla ya mipango ya matumizi ya ardhi 4,681, ikiwa ni pamoja na shughuli ya ugawaji wa hati za hakimiliki za kimila katika halmashauri ya Ushetu na vijiji vingine 48 vinavyoendelea kuandaliwa mipango hiyo katika halmashauri nyingine tano nchini.

Mpaka kukamilika kwake kutakuwa na mipango ya matumizi ya ardhi 4,729, kati ya vijiji 12,333 nchi nzima na kubaki vijiji 7604.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 26, 2025 na mkurugenzi wa mipango ya matumizi ya ardhi, usimamizi na uratibu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Jonas Masingija ameyasema hayo leo septemba 26, 2025, wakati wa uzinduzi wa shughuli ya ugawaji wa hati za hakimiliki za kimila kwenye vijiji vya Igunda na Butibu katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema uwepo wa hati za hakimiliki za kimila, umesaidia kuimarika kwa salama za miliki kwa wananchi hususani wale wanaoishi katika maeneo husika.

Ametaja manufaa ya nyaraka hizo kuwa ni pamoja na kupungua kwa migogoro ya ardhi nchini, kutengwa kwa maeneo mbalimbali ya matumizi ya ardhi ikiwemo ya makazi, kilimo, malisho ya mifugo, vyanzo vya maji, hifadhi za misitu, maeneo ya shule, masoko na taasisi nyingine kama ofisi ya kijiji na zahanati.

Aidha, Masingija ameishauri Halmashauri ya Ushetu kuangalia namna bora ya uwezeshaji ili vijiji vilivyosalia kwenye mpango huo vifikiwe.

Amesema: “Katika Kijiji cha Igunda, tumeandaa na kuwezesha utoaji wa hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi 595 na kijiji cha Bitibu ni wananchi 427, hivyo kufanya jumla ya wanufaika wa nyaraka hizi katika vijiji hivi viwili kufikia 1022 kwa leo.”

Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Ushetu, Denis Kakulima amesema atahakikisha halmashauri hiyo itaendelea kutenga bajeti katika kila mwaka ili wananchi wa vijiji vyote 112 viweze kufikiwa na kuandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi.

Amesema: “Halmashauri ya Ushetu ina jumla ya vijiji 112, ni vijiji 36 kati ya hivyo vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na kusalia vijiji 76. Halmashauri hii itahakikisha inaendelea kutenga bajeti ili kuweza kuvifikia vijiji vyote wananchi wake waandaliwe mpango wa matumizi ya ardhi.”

Mkazi wa Ushetu aliyenufaika na nyaraka hizo, Victoria Nathaniel amesema: “Tulikuwa tuna shida nyingi sana, migogoro ilikuwa haiishi, kupigana hakuishi, kuingiliana kwenye mipaka kila leo, tulikuwa tunahangaika sana mara kwa mtendaji kila siku, lakini leo tumefika mwisho baada ya kumilikishwa mashamba yetu.”

Naye Wilbert Malale, mkazi wa Butibu amesema: “Sasa hivi tutapata mikopo kwa urahisi kupitia hizi hati zetu, tunaishukuru sana serikali kwa hatua hii ni nzuri sana kwetu.”