Tanga. Waandishi wa habari mkoani Tanga wameshauriwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia kanuni kwenye kazi zao hasa kipindi hiki cha uchaguzi ili kujiepusha kuingia kwenye malumbano na vyombo vya dola wakiwa kwenye majukumu yao.
Akizungumza kwenye mdahalo wa ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Tanga kuelekea uchaguzi mkuu, uliofanyika leo Ijumaa Septemba 26, 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema endapo waandishi watazingatia kanuni na taratibu kwa kushirikiana na wadau, hatakuwa na tatizo.
Amesema Jeshi la Polisi linatambua na kuheshimu kazi za waandishi wa habari, hivyo limejipanga kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao katika hali ya usalama hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa ushirikiano mkubwa.
Mchunguzi amesema kwa kutambua umuhimu wa waandishi wa habari pamoja na majukumu yao, jeshi hilo litakuwa mstari wa mbele kulinda haki zao na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao bila hofu au vitisho muda wote wakiwa kazini.
Katika kipindi hiki cha uchaguzi, amewataka waandishi wa habari kutimiza wajibu wao wa kutoa taarifa kwenye jamiii, kwa kuzingatia sheria, miiko na maadili ya kazi zao kwani kufanya hivyo kutawasaidia kubaki salama kwenye mazingira ya kazi.
“Nawakumbusha kuhakikisha mnakuwa na utambulisho maalumu wa kuwatambulisha hususani maeneo ya mikutano ya kampeni na maeneo yatakayokuwa na vituo vya kupigia kura kwa kuvaa mavazi maalum au vitambulisho vya ithibati vitakavyotolewa na Bodi ya Ithibati Tanzania,” amesema Kamanda Mchunguzi.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Tanga (TPC), Lulu George amesema wataendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kufanya kazi zao kwa weledi hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kushirikiana na wadau wengine.
Amesema mwandishi wa habari akikumbushwa wajibu wake kwa kupewa mafunzo ya mara kwa mara, inasaidia kuweza kumkumbusha majukumu yake kwani na wao ni binadamu na huwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ukiacha zile za kazi.

Baadhi ya waandishi wa habari wakichangia kwenye mdahalo wa ulinzi na usalama wa waandishi wa habari mkoa wa Tanga,kuelekea uchaguzi mkuu. Picha na Rajabu Athumani
Kwamba yapo makosa ambayo wanafanya ila badala ya kukamatwa au kuchukuliwa kama makosa makubwa, mamlaka husika wanaweza kukaa chini na chombo na mwandishi husika kuweza kuweka sawa badala ya kuleta taharuki kwa kukamatana.
Amesema klabu za waandishi wa habari kwa sasa wanao mfumo maalumu wa kupeana mafunzo kwa waandishi wao, ni jinsi gani wanaweza kujiweka kwenye maeneo salama wanapokuwa kwenye kazi zao za kila siku.
Aidha, ofisa programu msaidizi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Edmund Kipungu amesema bado ipo changamoto ya waandishi wa habari, kutishwa na kunyimwa kutoa habari, hivyo kuomba mamlaka zote kutoka ushirikiano wa kuwa na uhusiano mzuri na waandishi ili kufanyakazi zao bila bughuza.
Amesema UTPC kwa kushirikiana na klabu za waandishi wa habari mikoani wanaendelea kuzungumza na wadau mbalimbali wa habari, kuona ni jinsi gani kila mdau atatoa mchango wake kuona waandishi wanapata ushirikiano kazini lakini bila kupata vitisho.
Mwanasiasa mkongwe Mkoa wa Tanga kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Mussa Mbaruku ameshauri waandishi wa habari kujiepusha na taarifa zinazoegemea upande mmoja kwani kwa kufanya hivyo inaweza kuleta changamoto kwenye jamii.
Mmoja wa waandishi aliyeshiriki mdahalo huo, Dominic Maro ameshauri waandishi kuunga mkono suala la kupata utambulisho wa Ithibati, kwani kwa kufanya hivyo ni rahisi kutambulika lakini mhusika kuweza kusaidiwa kwa kuonekana anafanyakazi kihalali.
Mafunzo hayo yamekwenda sambamba na kuweka mikakati kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga na waandishi kupeana ushirikiano katika kazi ili kila mmoja awajibike vizuri kwenye nafasi yake.