Yanga imesema imeshusha mzigo wa jezi mpya awamu ya pili zitakazokuwa na mabadiliko ili kuwakimbia wahujumu wa mapato wanaofyatua jezi feki.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema mwekezaji wa biashara ya jezi za klabu baada ya kumalizika kwa jezi za kwanza ameshtukia uwepo wa uzi feki mwingi sokoni.
Kamwe amesema baada ya kushtukia hilo wameamua kutengeneza jezi mpya zikazokuwa na alama tofauti mbili ambazo shabiki wa atakayekwenda kununua zitamsaidia kugundua kama anauziwa jezi feki au orijino.
“Jezi hizi mpya zitakuwa na tofauti hapa kulia. Jezi za sasa zina logo ya mdhamini, lakini hizi mpya zitakuwa na neno NIA kama ukienda kuzinunua ukakuta zina logo ya GSM kuanzia sasa tambua hiyo ni feki,” amesema.
“Alama ya pili wataona hizi jezi za sasa zina alama ya miaka ya Yanga ile 90 imeandikwa kwa juu, lakini ukigeuza ndani huioni lakini hizi mpya utaona hiyo 90N inaonekana kuanzia nje mpaka ndani.
“Ndugu zangu hii biashara ya jezi ina watu hatari sana. Tumejaribu sana kupambana nao, lakini bado tunaona kuna ugumu. Hivi tunavyoongea kuna makontena mengi ya jezi hizi za msimu huu tulizotangulia kuzileta zinaingizwa sokoni.
“Tukaona tulete jezi mpya ambazo zitakwenda kuipa klabu nguvu ya mapato yake kuliko kuendelea kuleta jezi zilezile ambazo zitakwenda kuwanufaisha watu wasioipenda hii klabu.”
Kamwe ameongeza kuwa tayari jezi hizo mpya zimeshaingia sokoni ambapo amewataka mashabiki wa Yanga kuzikimbilia ili kesho wapendeze uwanjani.