ADC kutoa mitaji kukuza uchumi wa wajasiriamali

Pemba. Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia  Chama cha Alliency For Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed  amesema  iwapo wananchi  watampa  ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, atawasaidia wajasiriamali na vijana kwa  kuwapatia mitaji itakayowawezesha kujiendesha kiuchumi na kukuza kipato chao.

Akizungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho katika  mkutano wa hadhara uliofanyika  Mtambwe Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba leo Septemba 27, 2025 mgombea huyo amesema Wajasirimali wamekuwa na kipato cha chini kutokana na kukosa mitaji.

Amesema iwapo wananchi watamchagua katika uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 ataweza kuelekeza nguvu zake katika kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapatia mitaji itakayo wawezesha kukuza kipato chao.

Amesema wajasiriamali wengi wanashindwa kujiendeleza kwa kukosa mitaji ya kuendeshea biashara zao, hivyo watakapo mchagua ataweza kuliangalia kwa karibu jambo hilo.

Pia, amesema kwa upande wa wavuvi ambao ni asilimia kubwa ya wakazi wa Visiwa Vya Zanzibar, akipata madaraka ataunda kamati maalumu itakayoangalia shida za wavuvi zipate kutatuliwa.

Hamad amesema pia serikali yake itashughulikia kilimo kwa kutafuta vifaa na pembejeo za kilimo kwa wakulima ili waweze kulima kilimo cha kisasa na kupata mavuno makubwa hasa kilimo cha mpunga.

‘’Mtakaponichagua kuwa rais nitawawezesha wajasiriamali na vijana kwa kuwapatia mitaji itakayowasaidia kuendesha biashara zao na kujikwamua na maisha,’’ amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu  wa chama hicho, Mwalimu Hamad Azani amesema endapo wananchi watakichagua chama hicho kitaondoa changamoto mbalimbali zikiwemo za maji na barabara.

Amesema baadhi vijiji vimekuwa na shida ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo Serikali ya ADC itahakikisha shida hizo zinaondoka.

‘’Mtakapotuchagua tutaziangalia changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yanakabiliwa na changamoto hiyo,’’ amesema Mwalimu.

Amesema mbali na changamoto hizo, pia watazingatia uboreshaji wa huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya katika maeneo ya vijiji vinavyoathirika, ili kupunguza wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.