Ahueni wakulima Kishapu wakikabidhiwa matrekta

Shinyanga.  Wakulima wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamekabidhiwa matrekta yenye thamani ya Sh238.4 milioni ili kuondokana na matumizi ya jembe la mkono na kuongeza uzalishaji kupitia kilimo na kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Akikabidhi matrekta hayo Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Peter Masindi leo Septemba 26, 2025 amesema hatua hiyo ni chachu ya kuwaletea wamiliki wa matrekta hayo ongezeko la kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa na kuondokana na umasikini.

Amesema matrekta hayo yametolewa kwa wakulima wanne  kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya NMB na kuwasisitiza wanapaswa kuwa mfano wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa  ya kilimo na siyo jembe la mkono na kutumia mifugo.

“Mikopo hii ya matrekta imetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia NMB kwa mikopo yenye  riba nafuu ya asilimia tisa, kayatumieni  kwa malengo ya kuongeza kipato cha familia na kukuza uchumi wenu,”amesema Mkuu wa Wilaya.

Amesema Serikali inatambua thamani ya mkulima kwa kuwa sekta ya kilimo ni mhimili wa pato la taifa, na hivyo wamiliki wa matrekta hayo wanapaswa kuwa mfano wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye kilimo.

 Amewataka wamiliki wa matrekta hayo kuwashirikisha vijana kwa kuwaeleza faida za kilimo cha kisasa kupitia zana hizo ili nao watumie fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya wakulima walionufaika na mkopo huo akiwemo Sagala Luminu mkazi wa Kishapu amesema walikuwa wanatumia jembe la kukokotwa na ngombe hali ambayo ilikuwa inafanya washindwe kulima zaidi kutokana na kutumia nguvu kubwa.

Mkulima mwingine Saba Kwihula mkazi wa Mwamalasa, ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa wakulima, ambapo matrekta hayo yatawasaidia kurahisisha shughuli za kilimo kwa kutumia muda mfupi kulima eneo kubwa.

 Meneja wa Benki ya NMB Wilayani humo, Alexander Gabriel Macheko amesema lengo la kutoa mikopo hiyo ni kusaidia kuinua sekta ya kilimo na kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.