Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi na kumwachia huru, Kelvin Lukoa (21), baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake.
Lukoa, alikuwa anakabiliwa na shitaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 110.10 kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo amefutiwa shtaka lake chini ya kifungu namba 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani mwaka 2020 na kusomewa shtaka hilo na kurudishwa rumande kutokana na shtaka lililokuwa linamkabili, kutokuwa na dhamana.
Hata hivyo kesi yake imeshafutwa mara mbili na DPP na kisha mshtakiwa huyo kukamatwa na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka kama la awali.
Uamuzi wa kumwachia huru mshtakiwa huyo, umetolewa jana, Ijumaa Septemba 26, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, baada ya DPP kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi yake.
Awali, kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali Roida Mwakamele aliieleza mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhini alimuuliza wakili wa mshtakiwa, Yohana Kibindo iwapo ana pingamizi.
Wakili Kibindo alidai kuwa hana pingamizi na ilikuwa ni ombi lake mteja wake afutiwe kesi kwa kuwa wakati anakamatwa mwaka 2020, alikuwa na umri wa miaka 16.

Mshtakiwa Kelvin Lukoa (mwenye tisheti rangi ya chungwa) akiwa chini ya askari magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kabla ya kuachiwa huru jana Septemba 26, 2025. Picha na Hadija Jumanne
“Mheshimiwa hakimu sina pingamizi juu ya hilo, lakini hii ni mara ya pili kwa DPP kumfutia kesi mteja wangu na kumkamata tena, naamini safari hii hatakamatwa tena,” alidai wakili Kibindo na kuongeza;
“Lakini pia, kesi hii ni ya muda mrefu na mara ya mwisho kutajwa Septemba 17, 2025, upande wa mashtaka uliomba niliwasilishe cheti za kuzaliwa cha mteja wangu ili kudhibitisha umri wake na leo nimekuja nacho hapa mahakamani, lakini kwa kuwa DPP ameleta ombi lake hana nia ya kuendelea na kesi hii, hivyo mimi sina pingamizi dhidi yake,” aliongeza Wakili Kibindo.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alisema kwa kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo, basi mahakama hiyo inamwachia huru mshtakiwa huyo na akawe raia mwema.
“Haya African Lukoa, kama ambavyo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini amesema hana nia ya kuendelea na kesi dhidi yako, basi mahakama hii inakuachia huru kuanzia sasa, sawa?” Alisema Hakimu Mhini.
Hakimu Mhini baada ya kutoa maelekezo hayo, mshtakiwa huyo aliishukuru mahakama kwa kuinamisha kichwa chini huku akikunja mikono yake miwili na kuiweka kifuani.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alipelekwa kituo cha Polisi Buguruni kwa ajili ya kwenda kuchukuliwa alama za vidole na pamoja na hatua nyingine kabla kuachiwa.
Mshtakiwa na ombi la umri mdogo
Septemba 17, 2025 wakili Kibindo aliwasilisha mahakamani hapo hoja, akidai kuwa mteja wake wakati anakamatwa alikuwa ni mtoto wa umri wa miaka 16.
Wakili Kibindo alidai mteja wake huyo alikamatwa mwaka 2020, akiwa na umri wa miaka 16, hivyo aliomba mahakama hiyo imwachie huru mshtakiwa huyo kwa madai ni mtoto na amekaa mahabusu kwa muda mrefu.
Vilevile kesi hiyo ni ya muda mrefu na upande wa mashtaka wameshindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji.
Akijibu hoja hiyo, wakili Roida aliiomba mahakama ielekeze mshtakiwa huyo apeleke cheti cha kuzaliwa mahakamani hapo, siku kesi hiyo itakapoitwa.
Hata hivyo, mahakama ilielekeza Septemba 26, 2025 kesi hiyo itakapoitwa mahakamani hapo, mshtakiwa kupitia wakili wake awasilishe cheti halisi (Original) cha kuzaliwa.
Lukoa alikuwa anakabiliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 34693 ya mwaka 2024 yenye shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya.
Mshtakiwa anadaiwa Februari 17, 2020 eneo la Tabata Sanene, lililopo wilaya ya Ilala, alikutwa akisafirisha kilo 110.10 za bangi, kinyime cha sheria.
Hata hivyo, upande wa mashtaka baada ya upelelezi kukamilika na kumsomea hoja za awali mshtakiwa (PH) uliieleza mahakama hiyo kuwa unatarajia kuwa na mashahidi wanane na vielelezo vinne kithibitisha shtaka hilo.