BAADA ya kipa wa TRA United, Fikirini Bakari kukaa nje wiki mbili akiuguza jeraha la taya alilovunjika katika mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga wakati wa maandalizi ya msimu huu, kwa sasa amejiunga kambini akipambania namba kikosi cha kwanza.
Fikirini alisema kwa sasa anaendelea vizuri, huku akiwa na tahadhari ya kuepuka kugongana na wenzake na anaamini ataendeleza ushindani wa namba katika nafasi yake.
“Kipindi cha wiki mbili nilichokuwa nje nilizingatia maelekezo ya daktari, nilikuwa nafanya mazoezi mepesi pia kupumzika kwa wakati na kula chakula nilichokuwa nimeelekezwa, hilo limemisaidia kuimarika kwa uharaka.
“Kwa sasa najituma na mazoezi ili niendelee kuwa fiti kuongeza ushindani utakaomshawishi kocha kuniamini kuanza katika kikosi cha kwanza,” alisema.
Mechi dhidi ya Dodoma Jiji iliyochezwa Septemba 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, Fikirini alikaa benchi huku golini akianza Jean Noel.
Katika mechi hiyo, mabao ya TRA United yalifungwa na Konate Fode dakika ya 58 na Joseph Akandwanaho dakika ya 81, huku Dodoma Jiji ikifunga kupitia Beno Ngassa dakika 52 na Idd Kipagwile kwa penalti dakika ya 85.
Fikirini yupo fiti kupambania namba TRA
