KOCHA wa Gaborone United, Khalid Niyonzima, amesema hawana presha yoyote kuelelea mchezo wa kesho dhidi ya Simba huku akiwahakikishia furaha mashabiki wa timu hiyo.
Gaborone United inaingia kwenye mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali itakayochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza nyumbani kwa bao 1-0 wiki iliyopita.
Kocha huyo amesema wapo tayari kuibuka na ushindi ugenini na kutinga hatua inayofuata huku akiweka wazi kwamba wataingia kwenye mechi hiyo wakiwa hawana cha kupoteza.
Amesema wanaifahamu Simba na wana matarajio makubwa kupata matokeo mazuri, huku akijivunia kikosi chake ambacho amekitaja kuwa kipo tayari kutoa burudani kikiwa hakina presha kutokana na kucheza bila ya mashabiki.
“Bao moja halifanyi kuwa chini tukiamini tumepoteza, kama wao walipata ushindi kwetu na sisi tutapata kwao, tunakutana na timu ambayo tunaifahamu, hatuna presha, tupo tayari kushindana.
“Wachezaji wanafahamu wanakutana na Simba ambayo imewafunga nyumbani na wao wamekuja kutafuta matokeo, hawatarajii mchezo rahisi, lakini mashabiki wa Gaborone watarajie furaha baada ya mchezo,” amesema Niyonzima.
Niyonzima amesema ana kikosi kizuri na bora ambacho kitaonyesha ushindani dhidi ya wapinzani wetu ambao wanaamini wataingia kwa presha kubwa kusaka ushindi.