Pretoria. Zikiwa zimetimia siku 252 tangu kufariki dunia kwa Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, mwili wake bado umehifadhiwa katika nyumba ya huduma za mazishi ya Two Mountains, Afrika Kusini kufuatia mvutano wa wapi azikwe, kati ya Serikali na familia yake.
Wakati mvutano huo ukiendelea, familia ya Lungu imetoka hadharani kukanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kwamba wameusafirisha kwa siri mwili huo kwenda nchini Hispania kwa ajili ya mazishi ya kificho.
Msemaji wa familia, Makebi Zulu, alisema kuwa familia haitatoa majibu kwa taarifa hizo ambazo hazina ukweli.
Lungu ambaye alikuwa Rais wa Zambia kuanzia Januari 26, 2015 hadi Agosti 24, 2021, alifariki dunia Juni 5, 2025 katika Hospitali ya Mediclinic Medforum mjini Pretoria, nchini Afrika Kusini, hadi sasa bado hajazikwa.
Kuchelewa kwa mazishi ya Lungu kutokana na mvutano wa wapi azikwe kiongozi huyo wa zamani wa Zambia. Familia inataka azikwe Afrika Kusini huku Serikali ikitaka azikwe nchini mwake kwa heshima zote za kiongozi wa kitaifa.
Ingawa Mahakama Kuu ya Pretoria nchini Afrika Kusini iliamuru mwili wa Lungu kurejeshwa Zambia kwa mazishi ya kitaifa, familia ya Lungu imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo, ikidai kuwa hauzingatii matakwa ya familia.

Uamuzi huo wa familia umesababisha kucheleweshwa kwa mchakato wa kurejesha mwili, huku mazungumzo rasmi na Serikali ya Zambia yakiendelea.
Kufikia Agosti 20, 2025, mwili wa Lungu bado ulikuwa umehifadhiwa katika nyumba ya huduma za mazishi za Two Mountains nchini Afrika Kusini.
Katika barua iliyotumwa kwa familia na Serikali ya Zambia, kampuni hiyo ilithibitisha kuwa mwili wa marehemu Lungu bado upo kwenye hifadhi, huku mgogoro kuhusu mahali pa mazishi ukiendelea.
Aidha, ilionya kuwa ingawa mwili umehifadhiwa kwa dawa maalumu, kuhifadhiwa kwa muda mrefu kunaweza kusababisha dalili fulani za kuharibika kwa mwili.

Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda (kushoto) na Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugambe
Chanzo cha mvutano huu kilianzia kwenye uhasama kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema, aliyemshinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa 2021. Lakini sasa mzozo huu umechukua sura mpya, ukiwa umejaa tuhuma nyingi zikiwamo za uchawi.
Mivutano kwa marais wengine
Nchini Angola, baada ya kifo cha Rais José Eduardo dos Santos, kilichotokea Julai 8, 2022 nchini Hispania, ulizuka mvutano wa wapi azikwe.
Rais João Lourenço na mke wa nne wa Dos Santos walitaka mwili wake urejeshwe nyumbani Angola kwa ajili ya mazishi ya kitaifa, hata hivyo uamuzi huo ulipingwa na binti aliyekuwa akiishi Hispania.
Binti wa Dos Santos, Welwitschia “Tchizé” dos Santos, alitaka mazishi ya kifamilia ya faragha na kaburi lisilojulikana sana huko Hispania, ili watoto wake (wajukuu wa Dos Santos) waweze kudhulu kaburi la babu yao.
Tchizé kwenye hoja zake alisisitiza kuwa alikuwa akiungwa mkono na baadhi ya ndugu zake ambao wanakabiliwa na tuhuma za ufisadi nchini Angola na huenda wakakamatwa iwapo watarudi.
Mtoto mwingine wa Dos Santos alitoa hoja kwamba Serikali haina wajibu wa kikatiba wa kushughulikia mazishi ya baba yao, na uamuzi huo unapaswa kuwa wa familia.
Pia, mwaka 2019, hali ya aina hiyo ilitokea nchini Zimbabwe baada ya kifo cha Robert Mugabe aliyeitawala nchini hiyo kwa miaka 37.
Wazimbabwe wengi walidhani Mugabe angezikwa katika eneo la makaburi ya mashujaa lililoko jijini Harare, lililojengwa wakati wa utawala wake (Mugabe).
Kufuatia kifo hicho, mrithi wake, Rais Emmerson Mnangagwa, alianza kujenga jumba la kifahari kwa ajili ya kumzika Mugabe katika jijini la Harare.
Hata hivyo, familia ya Mugabe walikataa mpango huo, wakieleza kuwa hawakukubaliana nao hasa kutokana na mazingira ya kuondolewa kwake madarakani.
Walidai kuwa Mugabe alisalitiwa na wafuasi wake wa karibu, akiwemo Mnangagwa mwenyewe.
Familia ilisema kuwa mwili ni wao, na baada ya wiki kadhaa za mvutano, walishinda kesi hiyo na Mugabe, shujaa mkuu wa harakati za ukombozi wa Zimbabwe, alizikwa katika kijiji chake cha nyumbani, bila kuwepo kwa mwakilishi yeyote wa Serikali.
Pia, Rais wa kwanza wa Zambia baada ya uhuru, Kenneth Kaunda, maarufu KK, pia alijulikana mtu wa amani hakuweza kupata mahali pa kupumzika bila mvutano kutokea.
Kwa mujibu wa familia, alitaka azikwe karibu na mke wake, na si katika eneo rasmi lililotengwa na serikali. Hata hivyo, KK alizikwa katika ‘Embassy Memorial Park’ jijini Lusaka.
Hata kwa Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah ambaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu huko Bucharest nchini Romania naye ulitokea mvutano wa mazishi yake.
Awali, Nkrumah alizikwa Conakry, Guinea, ambako alikuwa akiishi uhamishoni, lakini baadaye mwili wake ulirejeshwa Ghana ambako yalifanyika mazishi jijini Accra, na alizikwa katika kijiji chake cha asili, Nkroful.
Lakini, miaka kadhaa baadaye mabaki ya mwili wa Nkrumah yalihamishiwa na kuzika tena katika jumba la kumbukumbu lenye hadhi lilijengwa Accra, na mara kwa mara, familia yake huko Nkroful wamekuwa wakitoa kauli wakitaka mwili wake urejeshwe tena kwao.
Mwaka 2012, Rais John Evans Atta-Mills wa Ghana alifariki dunia akiwa madarakani, na hata kupata mahali pa kumzika haikuwa rahisi.
Baadhi ya wanafamilia walitaka azikwe kijijini kwao, lakini hoja hiyo haikuungwa mkono sana wakati huo.
Eneo la kwanza lililochimbwa kaburi kwa ajili ya mazishi yake liliachwa baada ya kutangazwa kuwa halifai. Hatimaye alizikwa kwenye bustani maalumu.
Makubaliano yalikuwa kwamba bustani hiyo itatumika kama sehemu ya mazishi ya marais wote wa Ghana.
Pia, alipofariki dunia Rais mwingine wa zamani wa Ghana, Jerry Rawlings, kulitokea mvutano kati ya familia na Serikali.
Rawlings hakuzikwa karibu na mahali alipolikwa Atta-Mills, bali familia yake kutoka kijijini kwao waliishutumu serikali kwa ‘kuhodhi mwili wake’.
Rawlings alizikwa katika makaburi ya kijeshi mjini Accra, kwa heshima zote za kijeshi.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.