Mechi za kujiuliza Ligi Kuu Bara

UHONDO wa Ligi Kuu Bara unaendelea leo kwa mechi mbili kupigwa ambapo saa 8:00 mchana, Pamba Jiji itaikaribisha TRA United kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku saa 10:15 jioni Mtibwa Sugar ikipambana na Fountain Gate.
Hizi ni mechi za kujiuliza kwa timu zote kwani hazijapata ushindi tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu. 
Kwa Pamba Jiji ni mechi ya kwanza nyumbani ila ni ya tatu msimu huu, baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo, Septemba 18, kisha kuchapwa na Yanga mabao 3-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Septemba 24.
Kwa upande wa TRA United zamani Tabora United, hii ni mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kikosi hicho kuanza kwa sare ya mabao 2-2 nyumbani, katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Septemba 20.
Msimu wa 2024-2025, pambano la mwisho lililopigwa Aprili 5, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Pamba Jiji ilishinda bao 1-0, ikiwa ni kisasi baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza Tabora United, sasa TRA United kushinda pia 1-0, Oktoba 23, 2024. 
Kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mtibwa Sugar iliyoanza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha bao 1-0, dhidi ya maafande wa Mashujaa Septemba 21, itakabiliana na Fountain Gate inayokabiliwa na changamoto ya ufinyu wa wachezaji kikosini humo.
Fountain iliyochapwa mechi mbili mfululizo, ilianza na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, kisha pia kuchapwa mabao 3-0 na Simba, ina ufinyu wa wachezaji baada ya nyota wapya ndani ya kikosi hicho kutokamilika kwa usajili wao.
Katika mechi dhidi ya Simba ambayo kikosi hicho kilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0, Septemba 25, timu hiyo ilikuwa na jumla ya wachezaji 13, ambapo walioanza ni 11 na waliokuwa benchi ni wawili tu, kutokana na wengine kutokamilika kwa usajili wao.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika Ligi Kuu, ilikuwa Machi 2, 2024, ambapo Mtibwa Sugar iliifunga Fountain Gate zamani Singida Fountain Gate 2-0, yaliyofungwa na Abdul Hillary kwa penalti dakika ya 70 na Omary Marungu dakika ya 76.
Akizungumza baada ya mechi na Simba, Kocha wa Fountain Gate, Denis Kitambi alinukuliwa akisema ufinyu wa wachezaji wa timu hiyo unampa wakati mgumu wa machaguo kikosini humo, ingawa bado nafasi wanayo ya kurekebisha mambo yanayotokea.
“Ni hatari kwa sababu unapokuwa benchi na wachezaji wawili tu unaombea wasiumie wengine, ni hatua ngumu tunayopitia kwa kweli na hata morali ya timu inashuka, bado ni mapema sana ingawa tunahitaji jitihada za ziada,” alinukuliwa Kitambi.
Kwa upande wa Kocha wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’, alisema licha ya kupoteza mechi ya kwanza, lakini wachezaji wa timu hiyo walicheza vizuri, japo wanatakiwa kuongeza umakini katika eneo la mwisho kutokana na nafasi zinazotengenezwa.