Mmmh! Diarra mtegoni Yanga | Mwanaspoti

KIPA namba moja wa Yanga, Djigui Diarra ameingia msimu wa tano akiitumikia timu hiyo aliyojiunga nayo msimu wa 2021-2022 akitokea Stade Malien ya Mali, huku akiweka utawala Ligi Kuu Bara na katika klabu hiyo kongwe nchini.

Licha ya kuweka utawala huo, lakini anakabiliwa na mtihani mzito katika mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola. Hiyo ni baada ya kuukwepa juzi dhidi ya Pamba Jiji.

Diarra ambaye ana tuzo mbili za kipa bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021-2022 na 2022-2023, katika mchezo dhidi ya Wiliete anatakiwa kumaliza bila ya kuruhusu bao ili kuweka rekodi mpya.

Raia huyo wa Mali aliyeanza vizuri msimu huu kama ilivyokuwa 2023-2024, amekaa langoni katika mechi tatu za kimashindano bila ya kuruhusu bao katika muda wa kawaida.

Diarra alianza kudaka mechi ya Ngao ya Jamii wakati Yanga ikiifunga Simba bao 1-0. Baada ya hapo, akakaa langoni kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete ikiwa ni mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi ya tatu kuondoka na clean sheet mfululizo ni dhidi ya Pamba Jiji, Yanga ikishinda mabao 3-0.

Mwanzo huo mzuri wa Diarra, ni kama ilivyokuwa msimu wa 2023-2024 na alidaka mechi tatu mfululizo za kimashindano bila ya kuruhusu bao.

Msimu huo wakati Yanga inafundishwa na Miguel Gamondi, timu hiyo ilianza na nusu fainali ya Ngao ya Jamii ikiichapa Azam mabao 2-0, kisha fainali ikatoka 0-0 dhidi ya Simba, lakini Yanga ikapoteza kwa penalti 3-1.

Baada ya hapo, Yanga ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Djibouti Telecom na kushinda mabao 2-0. Hadi hapo, Diarra alikuwa na clean sheet tatu mfululizo za kimashindano, akaja kutibua mechi ya marudiano dhidi ya Djibouti Telecom, Yanga iliposhinda mabao 5-1.

Ukiweka kando rekodi hiyo bora, takwimu zinaonyesha msimu wa 2021-2022 ambao ulikuwa wa kwanza kwa Diarra Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Nassredine Nabi, mechi ya kwanza tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United aliruhusu bao moja, Yanga ikifungwa 1-0. Pia marudiano akaruhusu tena katika kichapo cha 1-0.

Hata hivyo, alikuja kukaa imara kwenye michezo iliyofuatia akianza na Ngao ya Jamii Yanga iliposhinda 1-0 dhidi ya Simba. Kisha ikafuatia Ligi Kuu Bara matokeo yakiwa hivi; Kagera Sugar 0-1 Yanga, Yanga 1-0 Geita Gold, KMC 0-2 Yanga na Yanga 2-0 Azam. Mechi ya sita ya ligi dhidi ya Ruvu Shooting, akaruhusu bao moja kwenye ushindi wa 3-1.

Msimu wa 2022-2023, pia ilishuhudiwa mechi ya kwanza tu ikiwa ya Ngao ya Jamii, akaruhusu bao moja, Yanga ikiifunga Simba mabao 2-1.

Msimu uliopita 2024-2025, mechi ya kwanza ya msimu kwake ilikuwa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, Yanga ilishinda bao 1-0, akaondoka na clean sheet lakini akaipoteza kwenye fainali dhidi ya Azam, Yanga iliposhinda mabao 4-1.

Kuhusu kuendelea kuilinda ngome ya Yanga, beki wa timu hiyo, Israel Mwenda amesema: “Ni muhimu sana kuzuia timu isiruhusu mabao, hilo ni jukumu la kwanza safu ya ulinzi, safu ya ushambuliaji tunaiacha ifunge na kama yenyewe inafanya kazi yake vizuri, sisi huku nyuma tunahakikisha haturuhusu bao, hiyo inatupa kujiamini katika michezo mingine.”