Morocco aipania Gaborone, aahidi kuivusha Simba

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema anatarajia mechi ngumu na ya ushindani lakini wapo tayari kuhakikisha timu hiyo inavuka kwenda hatua inayofuata bila ya kuangalia walichovuna ugenini.

Morocco amepewa jukumu la kuiongoza Simba katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana itakayochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kocha huyo amekabidhiwa mikoba ya Fadlu Davids ambaye aliiongoza Simba mechi ya ugenini na kushinda bao 1-0, kisha akatimkia Raja Casablanca ya nchini Morocco.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Morocco amesema wanafahamu kwamba bado hawapo katika nafasi nzuri na tayari wamefanyia kazi makosa ya mechi ya kwanza ugenini, hivyo wanaamini kesho mechi hiyo itakuwa ni muhimu kwao kufanya vizuri.

“Bao moja ugenini sio la kujiamini sana nyumbani, kama wao waliruhusu na sisi tunaweza kufanya hivyo, kilichopo sasa ni kuhakikisha tutafanya kazi yetu kwa kuipambania timu ifanye vizuri.

“Sijawahi kupoteza kwenye mechi ya kwanza ya mashindano, naamini wachezaji wangu wapo tayari na watapambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri na kufuzu hatua inayofuata.

“Sina presha na sijawahi kuwa na presha kwenye mambo ya mpira, tumejiandaa na tunawaahidi mashabiki kuwa tutawapa furaha huko watakapokuwa lakini na wao watuombee,” amesema Morocco.

Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe, amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari na wanatarajia dakika 90 mpya ambazo zinawahitaji kupata ushindi ili kufikia malengo.

“Matarajio yetu msimu huu ni makubwa na ili kufikia hatua hiyo ni lazima kupata matokeo mazuri kwenye mechi za awali, tupo tayari kuhakikisha tunapambana na kupata ushindi.

“Matokeo yaliyopita tumeyasahau, tunaingia kupambania dakika 90 bora na za ushindi, kwetu matarajio ni kucheza mechi ngumu kwani hata wapinzani wetu wamekuja kutafuta matokeo lakini kitu tulichokiandaa tutakifanyia kazi Uwanja wa Mkapa,” amesema Kapombe.